WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umewatahadharisha wafanyabiashara wanaokiuka sheria kwa kuchezea mizani na vipimo kuwa utawafuatilia waliko na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, WMA umewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatumia vipimo vilivyohakikiwa na vyenye Lakiri ya Wakala wa Vipimo, ili kujikinga dhidi ya kupunjwa uzito halisi wa bidhaa wanazonunua kwa thamani ya fedha wanazolipa.
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa WMA, Christopher Mwakibinga,ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026), yanayoendelea katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
Mwakibinga amesema,WMA umejipanga kuhakikisha wafanyabiashara wanaokiuka sheria za vipimo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa ukiukwaji wa makusudi wa sheria ni uhalifu.
“Wanaovunja sheria kwa makusudi hao ni wahalifu. Taratibu za kisheria zipo na tumejipanga katika mikoa yote. Tutawafuata huko waliko na kuwachukulia hatua,”amesema.
Amesema,pamoja na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria, WMA utaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi na namna ya kutambua vipimo vilivyohakikiwa na Wakala huo.
Kwa mujibu wa Mwakibinga, WMA pia hufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumiwa na wafanyabiashara na viwanda, ikiwemo viwanda vinavyozalisha bidhaa za chuma kama mabati na nondo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha bidhaa zinazouzwa kwa vipimo vya urefu, uzito au ujazo zinakidhi viwango vilivyowekwa, kufuatia baadhi ya malalamiko ya wananchi kuhusu bidhaa hizo.
“Adhabu zimetajwa kwenye Sheria ya Vipimo. Rai yangu kwa wafanyabiashara ni kutii sheria bila shuruti. Tutawafuata huko huko na hata wananchi tutawafuata; hatutasubiri waje ofisini,”amesisitiza.
Aidha, Mwakibinga amesema kupitia Maonesho hayo ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki, WMA imetumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu vipimo sahihi, pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya Wakala huo katika kulinda maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara wanaofuata sheria.

More Stories
Wafanyabiashara watakiwa kupanua biashara zao
Bandari ya Dar yazidi kung’ara
VETA yaweka mkakati kufikia Dira ya Taifa 2050