September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miss Universe Tanzania, Hexagon zaingia ubia

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MASHINDANO ya Miss Universe Tanzania chini ya Millen Prive & Co. Lifestyle yameingia ubia wa kimkakati wenye thamani ya Sh milioni 200 na Hexagon Properties, kwa lengo la kuwawezesha washiriki kupata maarifa, ujuzi na fursa za kiuchumi na kitaaluma.

Katika ubia huo, washiriki 23 waliofika fainali watapata mafunzo kuhusu sekta ya mali isiyohamishika, ikiwemo mafunzo ya vitendo katika miradi mbalimbali.

Aidha, washindi watano watakaoteuliwa watapata fursa ya kusoma kozi ya mwaka mmoja ya Real Estate Challenge jijini Dubai na kuwa mabalozi wa programu hiyo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ubia huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Hexagon Properties, Godfrey Maduhu, amesema kampuni hiyo imetoa kiwanja eneo la Mwasonga, Kigamboni, kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Miss Universe Tanzania.

Alisema pia kampuni hiyo imetenga Sh milioni tano kwa ajili ya washiriki watakaofanya vizuri katika challenge ya kutengeneza maudhui yatakayowasaidia kujenga masoko na kupata wateja.

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Miss Universe Tanzania, Millen Magese, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya programu ya Empower Beyond the Crown, inayolenga kuwawezesha vijana kwa kuwapatia ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kujenga maisha na taaluma endelevu hata baada ya mashindano.

Programu hiyo inatekelezwa kupitia Empower Beyond Miss Universe Programme, Empower Beyond Masterclass na Empower Beyond Reality TV Series, inayorushwa kupitia Azam TV.