September 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMBF yatenga Bill.1 kwa uwezeshaji wa vijana 50

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

NMB Foundation (NMBF), ikishirikiana na Benki ya NMB, imetenga Sh bilioni 1 kwa uwezeshaji wa vijana 50 watakaojiunga na vyuo vikuu katika mwaka wa masomo 2026/27 kupitia Nuru Yangu Scholarship and Mentorship.

Maombi yote yatapokelewa kupitia tovuti ya NMB Foundation, foundation.nmbbank.co.tz, kuanzia leo hadi tarehe 18 Septemba 2026. Fursa hiyo inalenga Watanzania waliomaliza Kidato cha Sita mwaka huu kwa Daraja la Kwanza lenye pointi tatu hadi tano, wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kifedha.

Vijana watakaochaguliwa watagharamiwa ada, fedha za kujikimu, mafunzo kwa vitendo, malipo ya lazima ya chuo na vifaa vya kujifunzia, ikiwemo kompyuta mpakato. Pia watapata ushauri wa kitaaluma, mafunzo ya uongozi na maandalizi ya kuingia katika soko la ajira.

Katika awamu mbili zilizopita, NMBF imetumia zaidi ya Sh bilioni 2.1 kuwawezesha vijana 101. Kundi jipya litafanya idadi ya wanufaika kufikia 151. Maombi hayana gharama na hakuna mtu aliyeidhinishwa kuuza nafasi hizo.