Na Waandishi Wetu,TimesMajira Online-Dodoma
WAZIRI wa Fedha,Balozi Khamis Omar amewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Mikopo kwa Dhamana za Mali Zinazohamishika wa Mwaka 2026, unaolenga kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo inayotolewa kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana.
Akiwasilisha muswada huo bungeni jijini Dodoma,Balozi Omar amesema kutungwa kwa sheria hiyo kutasaidia kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa mikopo,kuimarisha usimamizi wa dhamana,kulinda haki za wakopaji na wakopeshaji pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha hapa nchini.
Ambapo amesema sheria hiyo inayopendekezwa inalenga kuongeza matumizi ya huduma za benki hapa nchini kutoka asilimia 22 mwaka 2023 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Balozi Omar amesema pia muswada huo unalenga kuongeza uwiano wa mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi dhidi ya Pato la Taifa kutoka asilimia 22.5 mwaka 2024 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030,sambamba na kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2030, kutoka asilimia 17.1 mwaka 2024.
Amesema,hatua hiyo ni muhimu katika kupanua wigo wa wananchi na wafanyabiashara kupata mikopo kwa kutumia mali zinazohamishika kama dhamana, badala ya kutegemea zaidi mali zisizohamishika kama vile ardhi na majengo.
Aidha Balozi Omar amesema,miongoni mwa changamoto zinazolengwa kutatuliwa na muswada huo ni kutokuwepo kwa mfumo wa pamoja wa usajili wa mali zinazohamishika zinazoweza kutumika kama dhamana, ambapo hali hiyo imekuwa ikisababisha mali moja kutumika kama dhamana kwa mikopo mbalimbali bila wakopeshaji wengine kuwa na taarifa, jambo ambalo linaweza kuchangia kuongezeka kwa mikopo chechefu katika sekta ya fedha.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa usimamizi na utaratibu wa pamoja wa mali zinazohamishika zinazoweza kutumika kama dhamana pamoja na kutokuwepo kwa utaratibu madhubuti wa utekelezaji wa haki za mkopaji na mkopeshaji wakati wa kuuza mali hizo.
Hata hivyo amesema,umuhimu wa kuweka utaratibu huo unatokana na ukweli kwamba baadhi ya mali zinazohamishika zinaweza kupoteza thamani ndani ya muda mfupi au kuharibika.
Amebainisha kuwa muswada huo umegawanyika katika sehemu kumi zinazoweka mfumo mpana wa kisheria wa matumizi,usajili,usimamizi na utekelezaji wa dhamana zinazotokana na mali zinazohamishika.

More Stories
Wasanii wahimizwa kuwa mabalozi wa utunzaji wa fedha
Serikali yaongeza ulinzi watoto dhidi ya ukatili mtandaoni
Serikali yahakikishia ajira wenye ulemavu