Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wasanii, watengeneza maudhui, waandaaji wa matukio na wadau mbalimbali wa sanaa kutumia ushawishi wao kuelimisha jamii kuhusu matumizi na utunzaji sahihi wa noti na sarafu, hatua inayolenga kupunguza gharama za uchapishaji na usambazaji wa fedha nchini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika semina iliyoandaliwa na BoT kwa ajili ya wasanii, Meneja wa Mawasiliano wa Benki hiyo, Victoria Msina, amesema wadau wa sanaa wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa wananchi kutokana na ushawishi walionao katika jamii.
“Wasanii na watengeneza maudhui wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe huu kwa jamii kupitia kazi zao. Tunahitaji kutumia ushawishi wao kuongeza uelewa kuhusu matumizi na utunzaji sahihi wa noti na sarafu,” amesema Msina.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti na Uchumi wa BoT, Dkt. Suleiman Misango, amesema utunzaji usio sahihi wa noti husababisha kuchakaa kwa haraka na hivyo kuongeza gharama za uchapishaji wa fedha mpya.
“Noti zinapochakaa kwa sababu ya matumizi na utunzaji usio sahihi, gharama za kuzibadilisha na kuchapisha nyingine huongezeka. Ni muhimu wananchi kutambua kuwa noti na sarafu ni alama muhimu za utaifa zinazopaswa kuheshimiwa na kutunzwa,” amesema Dkt. Misango.
Ameongeza kuwa BoT hufuatilia mzunguko wa noti mbalimbali ili kubaini muda wake wa matumizi kabla ya kuchakaa, huku akisisitiza umuhimu wa matumizi ya huduma za kibenki na njia za kielektroniki katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha taslimu.

Nao wasanii walioshiriki semina hiyo wameipongeza BoT kwa kuwapatia elimu hiyo, wameahidi kutumia majukwaa yao mbalimbali kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kutunza noti pamoja na sarafu.
Wamesema elimu hiyo itawasaidia kuwa mabalozi wa ujumbe huo kupitia muziki, maudhui ya mitandaoni, matukio na majukwaa mengine wanayotumia kuwafikia wananchi.


More Stories
Muswada wa Sheria ya Mikopo wawasilishwa bungeni
Serikali yaongeza ulinzi watoto dhidi ya ukatili mtandaoni
Serikali yahakikishia ajira wenye ulemavu