Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma
TAASISI ya Saratani Ocean Road (ORCI) imewataka wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, kuachana na imani na mila potofu zinazodai kuwa vidonda visivyopona vinasababishwa na kulogwa, badala yake wafike hospitalini kwa uchunguzi wa kitaalamu kwa kuwa huenda vikawa ni dalili za saratani.
Hivyo imesisitiza kuwa saratani ikigundulika mapema na mgonjwa kuanza matibabu kwa wakati, inatibika na kuongeza uwezekano wa kupata matokeo mazuri ya matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijijinhapa leo Agosti 19,2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya hiyo, Dkt. Diwani Msemo,amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na saratani, kwani kuchelewa kufika hospitalini kutokana na imani potofu kunaweza kusababisha ugonjwa kugundulika ukiwa katika hatua za juu.
Aidha amesema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara na kutumia huduma za uchunguzi wa awali wa saratani.
Vilevile Dkt.Msemo amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa na wa kimkakati katika Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa lengo la kuibadilisha kuwa kituo cha ubora wa huduma za saratani barani Afrika. Uwekezaji huo umejikita katika miundombinu, vifaa tiba vya kisasa, huduma za uchunguzi, tiba ya mionzi, rasilimali watu na mifumo ya kidijitali.
ORCI inaendelea na ujenzi wa Kituo cha Saratani Mbeya chenye thamani ya Shilingi bilioni 11, ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 57 na kinatarajiwa kukamilika Januari 2027 na kuanza kutoa huduma Julai mwaka huo. Kituo hicho kinatarajiwa kusogeza huduma za saratani karibu na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Taasisi hii inaendelea na ujenzi wa Multipurpose Oncology Building jijini Dar es Salaam wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 5.9, ambao umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026. Jengo hilo litakuwa na wodi, maeneo ya tiba ya kemikali, kliniki za saratani, maabara, famasia pamoja na ofisi za wataalamu.
“Katika kuongeza uwezo wa tiba ya mionzi, ORCI imekamilisha mradi wa Linear Accelerator wenye uwekezaji wa takribani Shilingi bilioni 7.9, huku mashine hiyo ikiwa tayari inatoa huduma. Pia, taasisi imenunua mashine mbili za Cobalt zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 4, huku ukarabati wa vyumba vyake ukigharimu Shilingi milioni 300 na mashine hizo zikitarajiwa kuanza kutumika rasmi ifikapo Septemba 2026,”amesema.
Akizungumzia kwa upande wa uchunguzi wa saratani ya matiti,amesema ORCI imenunua mashine mbili mpya za Mammography zenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 1.1. Mashine hizo zitaongeza uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina wa saratani ya matiti na kusaidia kugundua ugonjwa katika hatua za awali ili wagonjwa waanze matibabu kwa wakati.
“Taasisi pia imefunga mashine ya PET Scan yenye thamani ya Shilingi bilioni 18.2, inayotumika kusaidia kugundua saratani na kuonyesha iwapo imesambaa, huku Tanzania ikiwa nchi ya kwanza katika Afrika Mashariki na Kati kuwa na mashine hiyo. Vilevile, imefunga mashine ya tiba ya mionzi ya ELEKTA Harmony yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.3 pamoja na mashine ya SPECT yenye gharama ya Shilingi bilioni 1.5,”amesema.
Hata hivyo Dkt.Msemo amesema kuwa juhudi za kupeleka huduma karibu na wananchi zimejumuisha kampeni ya Tiba Mkoba iliyofika katika mikoa 15 na kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani kwa zaidi ya watu 200,000. Taasisi pia inaandaa kuanzisha vituo vipya vya saratani katika mikoa ya Mtwara, Kigoma na Arusha, huku huduma za upasuaji mkubwa zikitarajiwa kuanza Oktoba 2026 baada ya kukamilika kwa vyumba vya upasuaji.
Pamoja na hayo Taasisi hiyo imewasihi wananchi kutopuuza dalili zinazoweza kuashiria saratani, ikiwemo vidonda visivyopona, na badala yake kufika katika vituo vya afya kwa uchunguzi wa kitaalamu. ORCI imesisitiza kuwa saratani ikiwahiwa inatibika, hivyo ugunduzi wa mapema, uchunguzi wa mara kwa mara na kuanza matibabu kwa wakati ni hatua muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza mzigo wa saratani kwa wananchi na Taifa.

More Stories
Sound Beat and Soft yazindua duka la vifaa vya muziki Kariakoo
Kutoka Maabara hadi Sokoni: UDSM yabuni Saruji na Teknolojia rahisi za Ujenzi
Tanga kujiandaa kupokea Gesi Asilia kwa matumizi