August 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake Nkasi wanufaika na uwezeshaji sekta ya uvuvi

Na Israel Mwaisaka , Nkasi

Wanawake katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameendelea kunufaika na jitihada za kuwawezesha kiuchumi kupitia sekta ya uvuvi, hatua inayowawezesha kuongeza kipato, kuboresha maisha ya familia zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Miongoni mwa wanufaika ni Mgeni Edward Lubisha, mkazi wa Kata ya Kabwe, ambaye ni mmiliki wa vyombo vya uvuvi na mchakataji wa samaki.

Mgeni amesema kupitia mradi wa FISH4ACP, unaotekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO), na washirika kwa ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Wizara ya Mashirikiano ya uchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani(BMZ), amesema alipata mafunzo, vifaa vya uchakataji wa samaki pamoja na ujuzi wa ujasiriamali.

Ameongeza kuwa kabla ya kunufaika na mradi huo alikuwa akifanya biashara ya samaki kwa mtaji mdogo na kutumia mbinu duni za uchakataji, hali iliyosababisha uzalishaji mdogo na faida isiyoridhisha.

Hata hivyo Mgeni ameeleza kuwa kupitia mafunzo aliyopata na ushiriki wake katika vikundi vya TAWFA, VICOBA na TANFISH, ameweza kujifunza namna bora ya kuendesha biashara, kutunza kumbukumbu za biashara, kutumia fedha kwa ufanisi na kuongeza thamani ya bidhaa za samaki.

Mgeni amesema uwezeshaji huo umeongeza uzalishaji, umemsaidia kupanua soko la bidhaa zake na kuongeza kipato, hatua ambayo pia imechangia kuboresha maisha ya familia yake.

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Nova Mlowe, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kuwawezesha wanawake wanaojihusisha na sekta ya uvuvi kupitia mafunzo, mitaji na teknolojia za kisasa, kwa lengo la kuongeza tija na ushindani wa bidhaa za uvuvi

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Tumaini Kingu, amewahimiza wanawake kutumia fursa zilizopo kwa kujiunga na vikundi vya uwezeshaji, akieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kujenga uwezo wa kiuchumi, kuongeza kipato cha kaya na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa.

FISH4ACP ni mpango unaolenga kuimarisha minyororo ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa viumbe maji katika nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki, kwa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa njia endelevu.