Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Korogwe
JAMII ya wananchi wa Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wametakiwa kutunza mazingira na kuhakikisha dunia inabaki kwenye asili yake ili kukinufaisha kizazi cha sasa na kile kijacho.
Hayo yalisemwa Agosti 13, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Selemani Mwongozo kwenye Ufunguzi wa Mafunzo ya siku mbili ya Mradi wa Tunza Uumbaji (Care for Creation), yanayoshirikisha Kamati za Maliasili za vijiji, vikundi vya misitu, kikundi cha kilimo, watendaji wa vijiji, na madiwani wa kata mbili za Vugiri na Lewa.

Mwongozo amesema TFCG na Danmission wamewaletea mradi mwingine baada ya kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mradi wa FORLIVES kwa mwaka 2023 hadi 2025, lakini mradi wa sasa Tunza Uumbaji umekuja kuweka msisitizo wa jamii kuendelea kutunza mazingira, na kuhakikisha sehemu anbayo mazingira hayo yaliharibiwa, basi sehemu hiyo iweze kurudishiwa kwenye asili yake.
“Tulikuwa na mpango wa awali tuliutekeleza 2023-2025 ambao ni FORLIVES, na bahati nzuri tulioutekeleza ilikuwa ni sisi tuliopo hapa, na shughuli ni zile zile zitafanyika, utunzaji wa misitu, mazingira, vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabianchi. Na sasa umekuja kwa namna nyingine, lakini sio kama tunaanza sifuri kabisa, hapana, bali tuna cha kuanzia, na Danmission kupitia TFCG amekuja na mpango huu.
“Sasa tunachotakiwa kufanya ni kuweza kuendeleza kile tulichokianza, kwani Tanzania ina misitu mingi, lakini Danmission ametuamini baada ya kufanya vizuri mradi wa kwanza kupitia FORLIVES mwaka 2023- 2025. Ni jukumu letu kulinda, kutunza na kuhakikisha sehemu ambayo mazingira yaliharibika tunarudishia. Neno hili Tunza Uumbaji ni kubwa sana, hivyo sisi tunatakiwa kuhakikisha palipoharibika panarudishiwa ili atakaekuja akute asili ya uumbaji tangu mwanzo,”amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Idd Shebila amesema jukumu la kulinda misitu, mazingira, vyanzo vya maji, ikiwemo kuzuia uchomaji wa moto na kulinda maliasili za misitu ni la wananchi, hivyo mafunzo hayo iwe ni muendelezo wa kulinda misitu yetu na mazingira yetu ya asili.
Diwani wa Kata ya Vugiri, Ramadhan Mandia amesema mradi wa kwanza wa FORLIVES ulisaidia pakubwa kusaidia kurudishia mazingira ya asili ikiwemo misitu, vyanzo vya maji, mazingira, hivyo ujio wa Mradi wa Tunza Uumbaji utasaidia kuendeleza kile ambacho wananchi wameshakianzisha.
Diwani wa Kata ya Lewa, Zakharia Ngwilizi amesema pamoja na upya wake kwenye nafasi hiyo, ameona maendeleo yaliyofanywa na Mradi wa FORLIVES ni makubwa, kwani wananchi walijengewa uwezo wa kuweza kusimamia na kutunza mazingira yao.
Mratibu wa Mradi huo wa Tunza Uumbaji ambaye pia ni Meneja wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), chini ya ufadhili wa Danmission, Bettie Luwuge amesema malengo ya mafunzo hayo ni kuzindua rasmi Mradi wa Tunza Uumbaji na kuwapa uelewa Kamati ya Maliasili za Vijiji (VNRC’s), vikundi vya misitu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine muhimu, matokeo yanayotarajiwa, namna mradi utakavyotekelezwa, pamoja na majukumu na majukumu ya kila mdau.

“Kuimarisha uwezo wa Kamati za Maliasili za Vijiji (VNRC’s) na vikundi vya misitu katika kutumia viashiria, zana na taratibu za utoaji taarifa za ufuatiliaji wa misitu zinazozingatia ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya Tabianchi, ili kusaidia ufuatiliaji wa misitu inayoongozwa na jamii na usimamizi wa misitu unaoweza kuendana na mabadiliko ya mazingira na tabianchi” alisema Luwuge.
Luwuge amesema vijiji vinavyonufaika na mradi huo vipo vinne, ambapo kwa upande wa Kata ya Vugiri ni Kijiji cha Old Ambangulu, Bagamoyo na Vugiri, wakati Kata ya Lewa ni Kijiji cha Mashindei.






More Stories
Makamba ataka jamii ipate taarifa sahihi sekta ndogo ya umeme
Mradi wa mageuzi tansia ya maziwa kuongeza uzalishaji
Yanga yatwaa Ngao ya Jamii ,Simba chali