Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
CHAMA cha Ushirika Pachani AMCOS, kilichoko mkoani Lindi , kimeibuka na ushindi wa jumla wa kampeni ya Vuna na Mixx ya Mixx by Yas kwa Kanda ya Pwani Kusini, na kijishindia gari ya magurudumu matatu maarufu ‘Guta’
Makabidhiano ya zawadi hiyo yalifanyika wakati wa hafla ya Vuna na Mixx katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane, Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi hivi karibuni.
Hiyo imekuja baada ya wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara waliotumia huduma za Mixx kupokea malipo ya mazao yao kukabidhiwa zawadi mbalimbali, zikiwemo guta, pikipiki, simu janja na baiskeli kupitia kampeni hiyo.
Zawadi hizo zilikabidhiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohammed Mohammed, wakati wa Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mohammed amepongeza matumizi ya teknolojia katika kurahisisha huduma za kifedha kwa wakulima, akisema mifumo ya kidijitali ina nafasi muhimu katika kuongeza usalama wa malipo na kuwawezesha wakulima kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
“Tunapowezesha wakulima kupata malipo yao kwa njia rahisi na salama, tunawapa nafasi ya kupanga vizuri shughuli zao na kuwekeza zaidi katika uzalishaji.
“Ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia inawanufaisha wananchi, wakiwemo wakulima,” amesema Mohammed.
Kwa upande wake, Mkuu wa Yas Kanda ya Pwani Kusini, Fadhila Saidi, amesema Mixx imeendelea kurahisisha namna wakulima wanavyopokea fedha za mazao yao, hususan kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghalani.
Amesema, katika msimu wa 2025/26, zaidi ya Sh150 bilioni zililipwa kwa wakulima kupitia Mixx, huku zaidi ya Sh50 bilioni zikiwa tayari zimelipwa katika msimu wa 2026/27.
“Lengo ni kuhakikisha mkulima anapokea fedha zake kwa haraka, salama na kwa uwazi. Zawadi tunazotoa pia zina matumizi ya moja kwa moja katika shughuli zao; kwa mfano, guta na pikipiki zinaweza kuwasaidia katika usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kila siku,” amesema Fadhila.
Katika hafla hiyo, wakulima walikabidhiwa guta nne, pikipiki tano, simu janja sita pamoja na baiskeli, ikiwa ni sehemu ya zawadi za Vuna na Mixx kwa wakulima waliotumia huduma hizo katika msimu uliopita.
Mbali na kupokea malipo ya mazao, Fadhila amesema wakulima wanaweza kutumia huduma ya Kilimo Pesa kupata mikopo kwa ajili ya shughuli za kilimo, pamoja na Afya Mkulima, inayowawezesha kupata bima ya afya kwao na familia zao.
Baadhi ya wakulima waliopokea zawadi hizo, akiwemo Mohammed Chikawe, Hassani Mohammed na Issa Mtiko, wamesema zawadi hizo zimewapa hamasa ya kuendelea kutumia huduma za kidijitali katika kupokea na kusimamia fedha zinazotokana na shughuli zao za kilimo.
Wamesema matumizi ya malipo ya kidijitali yamewarahisishia kupata fedha zao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu au kutembea na fedha taslimu.
Fadhila amesema Mixx itaendelea kushirikiana na Serikali, vyama vya ushirika, AMCOS, wanunuzi wa mazao na wadau wengine ili kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuongeza matumizi ya huduma za kifedha kidijitali.


More Stories
Ajishindia Mil. 50 ‘Kila muamala bao la ushindi’
Watanzania zaidi ya 90 wanufaika ‘ ikiingia tu goli’
Yas yazindua msimu wa sita Zanzibar Marathon 2026