November 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AFDB kuipatia Tanzania Dola Milioni 26 za Mabadiliko ya Tabianchi

Na Mwananchi Wetu,TimesMajira

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kuipatia Tanzania dola za Marekani milioni 26 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari zake.

Ahadi hiyo imetolewa katika mkutano wa pembezoni kati ya benki hiyo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Antalya, Uturuki, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamad Masauni, ameishukuru AfDB kwa kuitikia kwa haraka wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa taasisi za kifedha kuongeza uwekezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo ulitolewa na Rais Samia wakati akihutubia Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (Antalya Leaders’ Summit), ambapo alizitaka taasisi za kifedha kuwezesha upatikanaji wa fedha, vifaa na teknolojia zitakazochochea utekelezaji wa hatua madhubuti za kukabiliana na athari za tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.

Akizungumzia ushirikiano huo, Masauni amesema AfDB imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kufadhili miradi ya kimkakati inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Mradi wa Ustahimilivu wa Vyanzo vya Maji vya Mto Mkondoa uliopatiwa dola za Marekani milioni 9.4.

Amesema mradi huo unalenga kulinda na kuimarisha vyanzo vya maji vinavyohudumia maeneo ya Gairo, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro ili kupunguza athari za mafuriko na ukame unaojirudia mara kwa mara.

Aidha, amesema AfDB imechangia dola za Marekani 400,000 kupitia dirisha la ufadhili wa utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na dola milioni 15 zilizowasilishwa kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa ajili ya kuimarisha ustahimilivu wa maeneo ya pwani.

Mbali na ufadhili wa kifedha, Masauni amesema benki hiyo imeendelea kuipatia Tanzania wataalamu na ushauri wa kiufundi katika kuendeleza sekta ya biashara ya kaboni, hatua inayolenga kuongeza fursa za uwekezaji wa kijani na kuhakikisha rasilimali za mazingira zinachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Ameeleza kuwa Serikali inathamini ushirikiano na mchango wa AfDB katika kutekeleza ajenda ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na imesisitiza dhamira ya kuendeleza ushirikiano huo kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu wa nchi, kulinda rasilimali za mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu yanawanufaisha Watanzania.

Ushirikiano huo wa kifedha, kiteknolojia na kitaalamu unatajwa kuwa muhimu katika kujenga Tanzania yenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uchumi endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.