August 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima,wafugaji wahimizwa kulinda shughuli zao kwa bima

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

WAKULIMA,wafugaji na wavuvi hapa nchini wamehimizwa kukata bima ili kulinda mitaji yao dhidi ya majanga mbalimbali na kuhakikisha shughuli zao zinakuwa endelevu. 

Wito huo umetolewa na wataalamu wa sekta ya bima walioshiriki katika  maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yaliofanyika Agosti 8,2026 katika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,ambapo wametoa elimu kuhusu umuhimu wa bima katika kilimo, ufugaji na uvuvi.

Ofisa Ubora kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) Kanda ya Ziwa Halfan Isango akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)walipotembelea Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Monica Kijuu amesema, kampuni hiyo inatoa bima ya kilimo na ufugaji ili kuwawezesha wakulima na wafugaji kufanya shughuli zao kwa amani, wakijua kuwa wanaweza kufidiwa endapo majanga yatatokea,majanga yanayoweza kuathiri kilimo ni pamoja na ukame, mvua nyingi, mafuriko, moto, wadudu na wanyama waharibifu.

Kijuu amesema,mkulima aliyekuwa anatarajia kupata, kwa mfano, magunia 100 ya mahindi lakini kutokana na majanga akapata magunia 50, akiwa na bima anaweza kufidiwa thamani ya mavuno aliyopoteza kwa mujibu wa masharti ya bima huku kwa  wafugaji, bima inahusu ng’ombe, kuku, ndege na mifugo mingine inayofugwa nyumbani, ambapo mfugaji anaweza kufidiwa endapo mifugo yake itaathiriwa na majanga au magonjwa.

Msimamizi wa Ofisi wa Kampuni ya Bima ya Alliance Mkoa wa Mwanza, Paulina Mpanduji, amesema kampuni hiyo inatoa bima ya kilimo na ufugaji ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na hasara zinazotokana na majanga kwani hali ya hewa haitabiriki na mkulima anaweza kupanda mbegu lakini mvua zikawa chache na kusababisha ukame, hivyo endapo alikuwa akitarajia magunia 20 na akapata gunia moja atafidiwa ile hasara.

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Monica Kijuu na waandishi wa habari(hawapo pichani)walipotembelea Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi

Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kanda ya Ziwa, Stella Marwa amesema,shirika hilo linatoa bima za ajali na maisha ikiwemo bima ya kilimo inayomkinga mkulima dhidi ya ukame, wadudu, mvua nyingi na majanga mengine yanayoweza kusababisha mavuno pungufu.

Marwa amesema NIC pia inatoa elimu kwa wavuvi wanaotumia vizimba na njia za kawaida, ambapo bima inaweza kulinda dhidi ya majanga kama magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kuua samaki au vifaranga,endapo mawimbi yataharibu nyavu au keji, mvuvi mwenye bima anaweza kufidiwa  na kurejea katika shughuli zake.

Amesema wavuvi wa mitumbwi pia wanapaswa kukata bima kwa ajili ya vyombo vyao na maisha yao, akieleza kuwa injini ya boti ikipata hitilafu mvuvi anaweza kufidiwa. Aidha, mvuvi akipata ajali ziwani na kufariki, familia yake inaweza kupata fidia huku akibainisha kuwa wavuvi wengi bado hawakati bima za vyombo vyao wala bima binafsi.

Pia amesema,bima ya mifugo inalinda wafugaji dhidi ya hasara mbalimbali, ikiwemo mifugo kuchinjwa kwa lazima kwa ushauri wa daktari. Alitoa mfano wa ng’ombe wa maziwa anayeshauriwa kuchinjwa, ambapo mfugaji anaweza kufidiwa, pamoja na mifugo inayopata madhara kutokana na kuumwa na nyoka au ajali.

Hata hivyo amesema,bima pia kunaweza kumsaidia mkulima, mfugaji au mvuvi kupata huduma za kifedha ikiwemo mikopo kutoka taasisi za fedha, kwa kuwa bima huongeza ulinzi wa dhamana huku pale hasara inapotokea, fidia humsaidia mhusika kurejesha mtaji na kuendelea na shughuli zake bila kulazimika kutafuta fedha nyingine za kuanzia upya.

Meneja wa NIC Kanda ya Ziwa Stella Marwa na waandishi wa habari(hawapo pichani)walipotembelea Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi

Kwa upande wake, Ofisa Ubora kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) Kanda ya Ziwa Halfan Isango amesema,mamlaka hiyo iliandaa Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane kwa kushirikisha kampuni mbalimbali ili kutoa elimu kuhusu bima za kilimo cha mazao, ufugaji na uvuvi wa kufuga.

Isango amesema,katika maonesho hayo, Kijiji cha Bima kimepokea wageni zaidi ya 4,000 na wengine wamefikiwa kupitia vyombo vya habari.Hivyo aliwahimiza wananchi kufika katika ofisi za kampuni za bima ili kupata elimu kuhusu namna ya kulinda mitaji yao dhidi ya majanga mbalimbali.

“Sekta ya bima, kama mamlaka, tunawahakikishia ni salama na unapokata bima tunahakikisha mlengwa analipwa kwa wakati na kiwango stahiki. Hivyo wakulima walinde kilimo chao kwa kukata bima,” amesema Isango.

Msimamizi wa kampuni ya bima ya Alliance na waandishi wa habari(hawapo pichani)walipotembelea Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi