August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo aitaka NIRC kukamilisha ugawaji wa Pampu za Umwagiliaji

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Kilimo,Daniel Chongolo, ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) na kuitaka kuhakikisha pampu za Umwagiliaji zilizotengwa kwa ajili ya wakulima zinagaiwa kuanzia Agosti 30 kwa wanufaika katika mikoa husika ili ziweze kutumika kuongeza uzalishaji wa mazao.

Chongolo ametoa maelekezo hayo leo alipotembelea banda la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika viwanja vya John Malechela, Nzuguni, mkoani Dodoma.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika upatikanaji wa teknolojia za Umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji, hivyo ni muhimu vifaa hivyo viwafikie wakulima kwa wakati ili viweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa.

Waziri Chongolo amepongeza jitihada za Tume katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali za Umwagiliaji nchini, zikiwemo usambazaji wa pampu na utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji inayolenga kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa ufanisi mwaka mzima.

Kwa upande wake, Salome Mallamia Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ameeleza kuwa Tume itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha pampu hizo zinawafikia wakulima watakao nufaika ndani ya muda uliopangwa, hatua itakayochochea ongezeko la uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima na kuendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia kaulimbiu ya “Tambua Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050.