Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
JAMII imetakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo yao kuhusu watoto wenye ulemavu wanaoshindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa viti mwendo na vifaa vingine saidizi vinavyowawezesha kufika shuleni.
Wito huo umetolewa Agosti 6, 2026 na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, wakati wa kukabidhi viti mwendo 14 kwa watu wenye ulemavu, wakiwemo watoto, jijini Mbeya.
Dkt. Tulia amesema changamoto kubwa ni ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu watu wenye ulemavu wanaohitaji msaada, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wa ngazi za mitaa.
“Toeni taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa, mtendaji wa mtaa, hata balozi awe na taarifa ili kurahisisha pale bendera ya upendo inapopita tujue tunaingia nyumba zipi. Wakati mwingine si kwamba mzazi hataki kushirikiana, bali amelemewa na hali ya kumlea mtoto mwenye ulemavu ambaye humtegemea kwa kila kitu,” amesema.
Amesema viongozi wa mitaa na kata wanapaswa kuwa na orodha ya watu wenye ulemavu katika maeneo yao ili fursa za misaada zinapopatikana ziwanufaishe wahitaji halisi kwa wakati.
Aidha, amewataka viongozi hao kutowasubiri wahitaji waanze kutafutwa pale misaada inapowasili, bali wawe tayari wana taarifa zao.
“Huenda miongoni mwa watakaopewa viti mwendo yupo mwanafunzi ambaye analazimika kubebwa kila siku kwenda shule. Kadri anavyokua, mzazi hawezi kuendelea kumbeba. Tukiwafahamu mapema, tunaweza kuwapa kipaumbele ili kila mtoto apate nafasi ya kwenda shule,” amesema.
Dkt. Tulia pia amewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo yao wanapobaini uwepo wa mtu mwenye ulemavu anayehitaji msaada ili taarifa hizo zifike kwa mamlaka husika.
Akizungumza katika hafla hiyo, mzazi wa mtoto mwenye ulemavu, Alinksya Mbembela, amesema mtoto wake Elisha Mbembela mwenye umri wa miaka tisa alipata ulemavu wa kichwa, mikono na miguu kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa ujauzito.
Amesema mtoto huyo hawezi kutembea wala kukaa mwenyewe, hali inayomlazimu kumbeba mgongoni muda mwingi au kumlaza anapochoka.
Ameongeza kuwa baba wa mtoto huyo hakushiriki katika malezi yake baada ya kudai hakumtaka mtoto huyo.
Kwa upande wake, Mlezi wa Kata ya Ilomba, Haruna Kasare, akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust, amesema watu wenye ulemavu 14 walitambuliwa kunufaika na viti mwendo hivyo, wakiwemo watoto saba, huku wengine wakiwa watu wazima.
Kasare amesema bado kuna changamoto ya kuwafikia wahitaji wote kutokana na ukosefu wa taarifa kutoka kwa viongozi wa maeneo yao, jambo linalochelewesha utoaji wa misaada kwa watu wanaostahili.

More Stories
T-CAMS yaleta mapinduzi sekta ya uwakala wa forodha
Mafuta ya zabibu yavutia Nanenane
Nanauka apongeza Kariakoo Kwa kuwezesha vijana Kibiashara