Na Joyce Kasiki, Dodoma
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imewahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo kuanzisha viwanda vya ndani vya kuzalisha dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi, ikieleza kuwa hatua hiyo itapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa TMDA Kanda ya kati, Sonia Mkubwa, alisema mamlaka hiyo iko tayari kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekezaji kuanzia hatua za awali za maandalizi ya michoro ya viwanda hadi mchakato wa usajili.
Alisema uwepo wa viwanda vya ndani utasaidia kuongeza upatikanaji wa dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vilivyo salama, bora na vyenye ufanisi, sambamba na kuimarisha sekta ya mifugo nchini.
Mbali na kuhamasisha uwekezaji, Mkubwa alisema TMDA inatumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na majukumu ya mamlaka hiyo katika kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa hizo.
Alieleza kuwa Kanda ya Kati ya TMDA inahudumia mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro na Iringa, hivyo maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja na kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa zinazohusu afya ya mifugo.
Mkubwa alisema TMDA huhakikisha dawa zote za mifugo zinazoingizwa nchini zimesajiliwa na zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo vikifuata kanuni za uzalishaji bora (Good Manufacturing Practices – GMP).
Aidha, alisema maabara za TMDA zinatambuliwa kimataifa na hufanya uchunguzi kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika duniani, jambo linaloongeza uaminifu wa matokeo ya vipimo vinavyofanyika nchini.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa pamoja na kuhakikisha watoa huduma wanazingatia sifa na weledi unaohitajika.
Kwa mujibu wa Mkubwa, usalama, ubora na ufanisi wa dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji na kuimarisha maendeleo ya sekta ya kilimo na mifugo nchini.

More Stories
UDOM yabuni kifaa cha Utrasound bila kutumia mtandao
Teknolojia mpya yainua tija zao la Pamba Tanzania
IFTz yaongeza tija kwa wakulima kupitia Teknolojia rafiki