Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imesema ina mabwawa 741 ya kufugia samaki yanayomilikiwa na wafugaji zaidi ya 385, huku shughuli hiyo ikiendelea kuongeza kipato cha kaya na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 5,2026 katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella, amesema halmashauri imeendelea kuwawezesha wafugaji kupitia mafunzo na huduma za ugani ili kuongeza tija katika sekta hiyo.
Amesema kwa mwaka halmashauri huzalisha takribani kilo 246 za samaki, huku aina zinazofugwa zaidi zikiwa ni sato (tilapia) na kambale.
“Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ina wafugaji wa samaki zaidi ya 385 na mabwawa 741 yaliyopo katika kata 21 kati ya kata 28 tulizonazo”amesema .
Katika kata ambazo bado shughuli hii haijaenea, maafisa ugani na maafisa uvuvi wanaendelea kutoa elimu ili kuongeza uelewa na kuimarisha ufugaji wa kisasa wa samaki,” amesema Yegella.
Aidha, amewahasisha wananchi kuwekeza katika ufugaji wa bata wa mayai, akisema umeonyesha kuwa fursa yenye tija kubwa ya kiuchumi.
“Wananchi wengi wamezoea kufuga kuku wa mayai, lakini katika Kata ya Utengule Usongwe tuna mfugaji mkubwa wa bata wa mayai. Bata mmoja anaweza kutaga mayai zaidi ya 100 kwa mwaka, hivyo ni fursa ambayo wananchi wanapaswa kuijifunza na kuitumia kuongeza kipato,” amesema Mkurugenzi huyo.
Yegella amesema Maonesho ya Nanenane yanalenga kuwapa wananchi nafasi ya kujifunza teknolojia na mbinu bora za kilimo, ufugaji, matumizi ya mbegu bora na uzalishaji wenye tija.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule, amesema amefurahishwa na mafanikio ya wajasiriamali wengi wanaoshiriki maonesho, akibainisha kuwa wengi wao wamewezeshwa kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
“Wafugaji wa samaki, wazalishaji wa mboga, wafugaji wa nyuki na wazalishaji wa mbegu waliopo hapa ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo. Ni jambo linaloonyesha kuwa uwekezaji wa halmashauri unaendelea kuleta matokeo chanya,” amesema Haule.
Ameongeza kuwa halmashauri imeamua kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mboga mboga kwa lengo la kuongeza mapato na kuanzisha mashamba darasa yatakayowasaidia wakulima kujifunza mbinu bora za uzalishaji.
“Ardhi ya Wilaya ya Mbeya ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao mbalimbali. Tukijikita katika mazao machache yenye tija na kuyazalisha kwa wingi, tutaimarisha soko la ndani na kuongeza mauzo katika masoko ya nje,” amesema.
Mmoja wa wananchi waliotembelea maonesho hayo, Lucy Adam, amesema amejifunza mbinu mbalimbali za kilimo cha mboga kwa kutumia mifuko na vichuguu pamoja na teknolojia bora ya ufugaji wa samaki, ambazo anaamini zitamsaidia kuongeza uzalishaji na kipato chake.

More Stories
IFTz yaongeza tija kwa wakulima kupitia Teknolojia rafiki
UWT yahimiza matumizi ya mikopo ya asilimia kumi
TMDA yahamasisha viwanda vya dawa za mifugo