August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chunya yajipanga kuenzi mila,Desturi na tamaduni

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imesema imejipanga kuendelea kuhifadhi na kuenzi mila, desturi na tamaduni za asili, ikiwemo utamaduni wa mavazi ya jadi yaliyokuwa yakivaliwa na mababu kabla ya Uhuru.

Hayo yalisemwa na Afisa Utalii wa Wilaya ya Chunya, Petro Haule, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Halmashauri hiyo kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Haule amesema moja ya vivutio vilivyopo katika banda hilo ni mavazi ya kale yaliyotengenezwa kwa magome ya miti, yakiwemo shati na suruali, ambayo yalikuwa yakivaliwa na mababu kama sehemu ya utamaduni wao.

Amesema lengo la kuonyesha mavazi hayo ni kuhamasisha jamii kujifunza na kuthamini mila, desturi na tamaduni za Tanzania badala ya kuiga tamaduni zinazopoteza maadili.

“Nguo hizi zilivaliwa na mababu zetu. Tumezileta kwenye maonesho haya ili jamii ijifunze na kuenzi utamaduni wetu. Wazee wetu walivaa mavazi yaliyokuwa yanastiri mwili na kuonyesha heshima kwa jamii,” amesema Haule.

Ameongeza kuwa Halmashauri imeamua kuendeleza elimu hiyo kutokana na kuongezeka kwa baadhi ya wananchi wanaovaa mavazi yasiyozingatia maadili na heshima ya jamii.

Mbali na mavazi ya jadi, Haule amesema Wilaya ya Chunya ina vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Mlima Mwene, ambao una historia na simulizi nyingi za kipekee zinazovutia wageni.

Kwa mujibu wake, mlima huo una mapango, mimea na wanyamapori wa aina mbalimbali, huku ukiwa pia na umuhimu kwa jamii katika kutabiri mvua na kuwasaidia wakulima kupanga shughuli zao za kilimo.

Amesema Mlima Mwene pia ni eneo muhimu kwa wanafunzi na watafiti kutokana na fursa za kufanya tafiti za mazingira, jiografia na urithi wa kitamaduni.

Aidha, amesema mila na desturi bado zinaendelea kuhifadhiwa katika eneo hilo, ambapo wazee wa kimila hukusanyika kufanya ibada na sala za jadi za kuombea mvua au kuondoa majanga mbalimbali yanayoweza kuikumba jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Dkt. Theodori Lucas, amesema wilaya hiyo ina vitalu vinne vya uwindaji wa kitalii vilivyopo katika maeneo ya wazi, pamoja na Mlima Mwene ambao una historia kubwa kwa kabila la Wasangu na unabeba urithi muhimu wa kitamaduni.

Naye mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Chunya, Elizabeth Kulwa, amesema maonesho ya mavazi ya magome ya miti yamewakumbusha namna mababu walivyokuwa wakithamini heshima na maadili kupitia mavazi yao.

Amesema ni muhimu kizazi cha sasa kujifunza historia hiyo ili kulinda utamaduni na maadili ya Kitanzania.