Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
WADAU wa kilimo wameeleza kuwa kilimo Ikolojia ni njia muhimu ya kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato kwao na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mdahalo maalum ulioandaliwa na Mtandao wa Mashirika Yanayojishughulisha na Utunzaji wa Bionuai Tanzania (TABIO), na wadau wengine wa masuala ya mbegu na kilimo ikolojia, uliofanyika katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Mdahalo huo ulilenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu kilimo ikolojia, kubainisha fursa zilizopo ikiwemo masoko, pamoja na kuhamasisha wadau kujisajili kushiriki mkutano wa Kilimo Hai Afrika utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mdau kutoka Jukwaa la Wanawake Vijijini Tanzania, linaloshirikisha nchi 11 za Kusini mwa Afrika, Judith alisema jukwaa hilo linafanya kazi na wanawake wakulima wadogo wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula na biashara huku likiwahamasisha kutumia kilimo ikolojia ili kuhakikisha usalama wa chakula.
Amesema kupitia jukwaa hilo wanawake wanapata fursa ya kubadilishana maarifa, teknolojia na mbegu za asili zinazozalishwa kwa kutumia mbinu za kilimo ikolojia.

“Jukwaa hili limetupa nafasi ya kujifunza kutoka kwa wakulima wenzetu wa nchi nyingine. Kubadilishana mbegu na uzoefu kumetusaidia kuongeza uzalishaji na kuhifadhi aina mbalimbali za mbegu zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi,” amesema Judith.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kilimo Hai Afrika (AFRONET), Mgeta Daud, amesema shirika hilo ni mlezi wa mashirika ya miavuli ya kilimo hai barani Afrika na huandaa mkutano wa Kilimo Hai Afrika kila baada ya miaka mitatu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao (TABIO), Abdalah Ramadhani Mkindi, amewataka maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kuhusu kilimo kisichotumia kemikali za viwandani na badala yake kuhamasisha matumizi ya mbinu rafiki za kilimo ikolojia.

Pia ameiomba Serikali kutambua mbegu za wakulima kutokana na mchango wake katika utunzaji wa mazingira, kuboresha lishe na kuongeza fursa za masoko.
Naye Mratibu wa Miradi ya Utafiti na Sera kutoka SWISSAID, Gladness Martin, amesema tafiti shirikishi zinawapa wakulima uelewa wa kutambua thamani ya mbegu za asili na kuzihifadhi ili ziendelee kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

More Stories
IFTz yaongeza tija kwa wakulima kupitia Teknolojia rafiki
UWT yahimiza matumizi ya mikopo ya asilimia kumi
TMDA yahamasisha viwanda vya dawa za mifugo