August 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mbarawa ashuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya TRC

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Agosti 5, 2026, ameshuhudia hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya FS Engineering na ITS Engineering za Italia, hafla iliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Miundombinu na Uchukuzi ya Italia jijini Rome

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia,Edoardo Rixi, ambapo Hati ya Makubaliano ilisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Masanja , Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa FS Engineering, Dkt. Dario Lo Bosco, pamoja na Mkurugenzi wa ITS Engineering, Michele Titton

Makubaliano hayo yanaweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya pande hizo katika kuendeleza miradi ya reli, miundombinu na mifumo ya usafiri nchini Tanzania kupitia kubadilishana utaalamu, teknolojia na uzoefu wa kitaalamu.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha uendelezaji wa miundombinu endelevu, kuongeza ufanisi wa mifumo ya usafiri na kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi

Kupitia makubaliano hayo, FS Engineering itatoa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya usanifu na uhandisi, kufanya tafiti za upembuzi yakinifu, tathmini za kiufundi na kimkakati pamoja na kuandaa suluhisho bunifu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya reli na usafirishaji.

Aidha, kampuni hiyo itaishirikisha Tanzania kwenye teknolojia za kisasa katika maeneo ya kidijitali, usalama wa miundombinu, uendelevu wa miradi na ubunifu wa kiteknolojia

Moja ya maeneo muhimu ya ushirikiano ni matumizi ya Digital Control Room, mfumo wa kisasa wa FS Engineering unaowezesha ufuatiliaji wa miradi mikubwa ya miundombinu kwa wakati halisi kwa kutumia teknolojia za kidijitali, ndege zisizo na rubani (drones) na uchambuzi wa taarifa (data analytics), hatua itakayoongeza usalama, ufanisi wa utekelezaji wa miradi na ubora wa maamuzi ya kiufundi

Wakizungumza baada ya hafla hiyo, viongozi wa pande zote wameeleza kuwa makubaliano hayo yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa.