*Petroli ya shuka kwa sh.92,dizeli sh.204
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA),imetangaza bei ya mafuta itakayotumika hapa nchini kuanzia Jumatano, Agosti 5, 2026 huku ikionesha ahueni kwa wananchi baada ya bei hizo kushuka kwa kiasi.
Ambapo bei ya petroli imeshuka kwa sh.92 kwa lita,dizeli imeshuka kwa sh.204 kwa lita huku mafuta ya taa yakushuka kwa sh.440 kwa lita,hali ambayo itawapa unafuu wa gharama za maisha kwa wananchi, wamiliki wa vyombo vya usafiri,mitambo na viwanda.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA),Salum Mnuna, inaonesha kuwa, kwa mwezi Agosti 2026, Dar-es-Salaam petroli itauzwa kwa sh.3,898, Tanga sh.3,959 na Mtwara sh.3,990.
Aidha, dizeli itauzwa sh.3978 kwa Dar-es- Salaam, sh.4,039 Tanga na sh.4,070 Mtwara. Kwa upande wa mafuta ya taa, kwa Dar-es-Salaam sh.4,003,Tanga sh.4,065 na Mtwara sh.4,096, mtawalia.
Mnuna amevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei husika, punguzo, na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika cha mafuta sanjari na kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na EWURA.
“Ni kosa kisheria kutotekeleza maagizo haya na adhabu kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka,”amesisitiza Mnuna.
Ikumbukwe kuwa, EWURA hutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kila Jumatano ya kwanza ya mwezi ambazo hutumika kwa mwezi husika. Katika miezi ya hivi karibuni, bei za mafuta zimekuwa zikibadilika mara kwa mara kutokana changamoto mbalimbali ikiwemo vita inayoendelea eneo la Mashariki ya Kati.
Mwisho

More Stories
Msajili wa Hazina akutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa EADB
Tanzania mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani
Chatanda ahamasisha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030