Na Joyce Kasiki,Dodoma
CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Pwani kimefanikiwa kubuni jokofu maalumu litakalowasaidia wakulima wa parachichi kuhifadhi mazao yao kwa muda mrefu, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa mazao unaotokea baada ya mavuno.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, mwalimu wa fani ya majokofu na viyoyozi wa VETA, Haji Sinani, alisema ubunifu huo ulianzishwa kufuatia maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore.
Alieleza kuwa baada ya kutembelea maeneo yanayozalisha parachichi kwa wingi, mkurugenzi huyo alibaini changamoto ya kuharibika kwa mazao hayo kabla ya kufika sokoni.
Kwa mujibu wa Sinani, wataalamu wa VETA walishirikiana na ofisi za kanda kubuni teknolojia hiyo na kufanya majaribio yaliyothibitisha kuwa jokofu hilo lina uwezo wa kuhifadhi parachichi kwa muda mrefu bila kupoteza ubora wake.
Alisema teknolojia hiyo itawapa wakulima nafasi ya kusubiri masoko yenye bei nzuri badala ya kulazimika kuuza mazao yao haraka kwa hofu ya kuharibika. Aliongeza kuwa parachichi mabichi yanaweza kuhifadhiwa kwa kipindi cha miezi mitatu hadi mwaka mmoja, huku yale yaliyoiva yakidumu kati ya wiki mbili na mwezi mmoja.
Aidha, alifafanua kuwa jokofu hilo limeundwa kufanya kazi katika kiwango cha joto cha nyuzi 4 hadi 8 za Selsiasi, ambacho kinafaa kwa uhifadhi wa parachichi. Mfumo wake pia hujiendesha kiotomatiki kwa kuwasha na kuzima kulingana na kiwango cha joto kilichowekwa.
Kwa sasa, VETA inaendelea kukamilisha hatua za mwisho za majaribio ili kuhakikisha teknolojia hiyo inafanya kazi kwa ufanisi kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa na wakulima nchini.

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali
VETA Singida yahamasisha utengenezaji bora wa Silaji Tanzania