Na Joyce Kasiki, Dodoma
CHUO cha Ufundi Stadi Tanzania (VETA) Singida kimewahimiza wafugaji nchini kujifunza teknolojia ya kutengeneza silaji ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora cha mifugo wakati wa kiangazi, hatua itakayoongeza uzalishaji wa maziwa na nyama pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma, Mkufunzi Mwandamizi wa Chuo cha VETA Singida, Dkt. Chrispin Mkopi, amesema chuo hicho, mbali na kutoa mafunzo ya fani mbalimbali za ufundi, kinafundisha pia fani ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji na kimefika maoneshoni kikiwa na bidhaa mbalimbali zilizochakatwa na wanafunzi pamoja na wakufunzi wake.
Amesema moja ya teknolojia inayotolewa na chuo hicho ni utengenezaji wa silaji, ambao hutumia majani ya mahindi au nyasi maalumu aina ya Elephant Grass zinazovunwa, kukaushwa kwa muda mfupi na kisha kuvundikwa kwenye shimo au mifuko maalumu isiyopitisha hewa ili kuchachushwa kwa siku 21.
Dkt. Mkopi amesema ili kuongeza ubora wa lishe, majani hayo huongezewa viambato mbalimbali kama molasesi na pumba za mahindi, hatua inayoongeza thamani ya chakula hicho na kukifanya kuwa na virutubisho vinavyohitajika na mifugo.
“Silaji ni muhimu sana wakati wa ukame ambapo upatikanaji wa malisho huwa mdogo. Chakula hiki huongeza uzalishaji wa maziwa kwa ng’ombe wa maziwa na pia huongeza uzito wa ng’ombe wa nyama ndani ya kipindi kifupi cha takribani miezi mitatu, hivyo kuwafanya kufikia uzito unaohitajika kwa ajili ya soko,” amesema.
Amefafanua kuwa silaji inaweza kuhifadhiwa kwa kipindi cha hadi mwaka mmoja bila kupoteza ubora wake ikiwa imeandaliwa kwa kufuata taratibu sahihi za uchakataji na uhifadhi.
Dkt. Mkopi amewaalika wafugaji kutoka maeneo mbalimbali nchini kutembelea Chuo cha VETA Singida ili kupata mafunzo ya utengenezaji wa silaji na teknolojia nyingine za kisasa za uzalishaji wa mifugo, akisema mafunzo hayo hutolewa kwa muda wa kuanzia wiki mbili hadi miezi mitatu kulingana na mahitaji ya mshiriki.
Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa chakula cha mifugo ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza tija, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha sekta ya mifugo nchini.

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali