Na Joyce Kasiki, Timesmahira,Dodoma
CHUON Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimekuja na teknolojia bunifu za ufugaji wa samaki zinazotumia maji na eneo dogo, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za ufugaji na kuimarisha uchumi wa buluu nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutoka Shule Kuu ya Sayansi Asilia na Teknolojia ya Uvuvi, Ndalo Missana, amesema teknolojia hizo zimebuniwa ili kuwasaidia wafugaji kuongeza tija kwa kutumia rasilimali chache huku wakilinda mazingira.
Amesema moja ya teknolojia hizo hutumia mfumo unaochuja na kusafisha maji wakati samaki wakiendelea kufugwa, hivyo kupunguza matumizi ya maji na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
“Teknolojia hii inamwezesha mfugaji kutumia maji kwa kiwango kidogo lakini bado kupata uzalishaji mkubwa wa samaki,maji yanaendelea kusafishwa ndani ya mfumo, jambo linalopunguza gharama na kuongeza tija,” anesema Missana.
Ameongeza kuwa chuo pia kimebuni mfumo mwingine wa ufugaji unaobebeka ambao unaweza kuhamishwa kwa urahisi kulingana na mahitaji ya mfugaji na una uwezo wa kufugia samaki katika vizimba vitatu kwa wakati mmoja, hivyo kurahisisha uvunaji na kuongeza kipato.
Mbali na ubunifu wa teknolojia hizo, amesema Shule ya Sayansi Asilia na Teknolojia ya Uvuvi inaendelea kuzalisha vifaranga bora vya samaki pamoja na chakula chenye ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha wafugaji kuongeza uzalishaji na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Serikali katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.
Missana amesema chuo kinaendelea kuwafikia wafugaji kupitia maonesho mbalimbali ikiwemo Nanenane, Sabasaba na maonesho yanayofanyika chuoni, sambamba na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa kuwafuata wafugaji mashambani au kuwakaribisha chuoni kwa mafunzo.
Ameeleza kuwa teknolojia hizo ni matokeo ya tafiti na ubunifu wa wahadhiri kwa kushirikiana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hatua inayochangia kuwajengea wanafunzi uzoefu wa vitendo huku matokeo ya tafiti yakitatua changamoto za jamii.
Aidha, amesema baadhi ya mifumo hiyo hutumia mimea maalumu kusafisha maji yanayotumika kufugia samaki, jambo linaloongeza uendelevu wa mazingira na kuifanya teknolojia hiyo kuwa rafiki kwa wafugaji wa kisasa.
Kwa mujibu wa Missana, mwitikio wa wananchi katika Maonesho ya Nanenane umeonyesha kuwa teknolojia hizo zimeanza kuvutia wafugaji wengi wanaotaka kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbinu za kisasa.
“Tunaendelea kupokea wageni wengi wanaokuja kujifunza. Hii inaonyesha kuwa wafugaji wameanza kuona umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na kipato katika shughuli za ufugaji wa samaki,” amesema.

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali