Na Joyce Kasiki,Dodoma
WAKULIMA na wafugaji wametakiwa kuongeza matumizi ya bima ya kilimo na mifugo ili kujikinga na athari za hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi, magonjwa na majanga mengine yanayoathiri uzalishaji.
Wito huo umetolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), ambayo imeeleza kuwa bima ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaendelea kuwa na uhakika wa kiuchumi pindi wanapokumbwa na changamoto zinazoweza kuathiri shughuli zao.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya 33 ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dk. John Malecela Nzuguni jijini Dodoma, Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TIRA, Anna Massao, alisema sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto nyingi zinazoweza kusababisha hasara kubwa kwa wazalishaji.
Alisema matukio kama ukame, mvua kubwa, mafuriko, magonjwa ya mimea na mifugo yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji, hivyo bima inasaidia kutoa nafuu ya kifedha kwa mkulima au mfugaji anapopata hasara.
“Bima ya kilimo na mifugo inampa mkulima na mfugaji ulinzi dhidi ya majanga yanayoweza kuvuruga uwekezaji wao. Ni muhimu wananchi kuelewa kuwa bima si gharama pekee, bali ni kinga ya mali na kipato chao,” alisema.
Massao alisema kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane, TIRA inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za bima na namna zinavyoweza kutumika katika kulinda shughuli za uzalishaji.
Alifafanua kuwa kwa upande wa mifugo, bima husaidia kukabiliana na hasara zinazotokana na vifo vya mifugo, magonjwa, wizi na matukio mengine yanayoweza kuathiri wafugaji.
Aidha, alisema wananchi wanaotembelea banda la TIRA katika maonesho hayo wanapata fursa ya kupata elimu moja kwa moja kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya bima, wakiwemo Shirika la Taifa la Bima (NIC), Umoja wa Makampuni ya Bima za Kilimo Tanzania (TAIC) pamoja na kampuni nyingine zinazotoa huduma hizo.
Mbali na elimu ya bima, Massao alisema wananchi pia wanaweza kupata huduma kupitia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania, inayosaidia kushughulikia changamoto na malalamiko yanayohusiana na huduma za bima.
Aliwataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Nanenane kupata uelewa zaidi kuhusu huduma za bima ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kulinda uwekezaji wao katika kilimo na ufugaji.

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali