Na Joyce Kasiki, Dodoma
KAMPUNI ya Imara Tech imesema imefanikiwa kuuza zaidi ya mashine 2,500 za kilimo na mifugo ndani na nje ya Tanzania, huku ikifikia zaidi ya wakulima 100,000 na kupanua soko katika nchi nane za Afrika, mafanikio ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Mkurugenzi wa kampuni hiyo amesema wazo la kuanzisha Imara Tech lilianza mwaka 2015, ambapo wabunifu watatu walipata ruzuku ya awali ya Sh milioni 20 kutoka COSTECH kwa ajili ya kutengeneza mfano wa kwanza wa mashine yao ya kuchakata mazao.
Amesema baada ya mashine hiyo kufanyiwa majaribio na kuthibitika kukidhi mahitaji ya soko, kampuni ilipata ruzuku nyingine ya Sh milioni 40 kutoka COSTECH iliyowezesha kufanya utafiti wa soko kabla ya kuanzishwa rasmi mwaka 2019.
“Tulianza tukiwa wabunifu watatu pekee, lakini leo tuna wafanyakazi zaidi ya 50 na tumesambaza mashine zaidi ya 2,500 ndani na nje ya nchi. Tayari wakulima zaidi ya 100,000 wanatumia teknolojia zetu,” amesema.
Ameeleza kuwa kupitia usaidizi wa COSTECH alipata fursa ya kwenda Finland kukutana na wawekezaji, jambo lililozaa uwekezaji wa zaidi ya Sh milioni 500 uliosaidia kukuza shughuli za kampuni hiyo.
Kwa sasa kampuni hiyo inatekeleza mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza mashine za kilimo na mifugo jijini Dodoma, ambacho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa vikubwa Tanzania na Afrika Mashariki.
Kuhusu bidhaa zake, amesema mashine kuu ya Imara Tech ina uwezo wa kukoboa na kukoboa mazao tisa tofauti ikiwemo mahindi, maharage, mtama, mbaazi, alizeti, choroko na ulezi, huku pia kampuni ikizalisha mashine za kutengeneza chakula cha mifugo zinazokata mabua, kusaga magunzi na kuchanganya malighafi mbalimbali.
Aidha, amesema kampuni hiyo imeuza zaidi ya mashine 300 nje ya Tanzania, zikiwemo mashine 100 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, 75 Rwanda, 30 Zimbabwe, 16 Kenya, saba Malawi, sita Uganda na tano Burundi.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano na mashirika ya maendeleo yanayotekeleza miradi ya kilimo katika nchi mbalimbali pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zake, huku ubora wa mashine zinazochakata mazao tisa kwa wakati mmoja ukiwa kivutio kikubwa kwa wateja.
Hata hivyo, amesema kampuni bado inakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa wataalamu wa kuendesha mashine za kisasa za uzalishaji, hali inayowalazimu kuleta wakufunzi kutoka China, pamoja na gharama kubwa za uzalishaji zinazotokana na kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye malighafi licha ya mashine hizo kusamehewa kodi zinapouzwa kwa wakulima.
Ameongeza kuwa mashine hizo zimekuwa chanzo cha ajira kwa vijana, kwani mashine moja ina uwezo wa kuchakata hadi magunia 25 ya mazao kwa saa kwa kutumia lita moja tu ya mafuta, hivyo kumwezesha mjasiriamali kupata kipato cha takribani Sh 25,000 kwa saa kabla ya gharama za uendeshaji.

More Stories
Mwanafunzi abuni Lishe Bora kupambana na utapiamlo
VETA yaleta suluhisho uharibifu wa Parachichi
Mahundi awataka vijana kukemea uchochezi na kuitetea serikali