August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji wa mkutano wa Wanahisa wa Africa50, Jukwaa la miundombinu Afrika

Na Penina Malundo,Timesmajira

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 (General Shareholders’ Meeting – GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), utakaofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 1,200 kutoka Afrika na sehemu nyingine duniani, wakiwemo viongozi wa serikali, wawekezaji, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na mwenyekiti wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, unaolenga kuimarisha ushirikiano na kuvutia uwekezaji katika miradi ya miundombinu barani Afrika.

Balozi Omar alisema Africa50, iliyoanzishwa mwaka 2013 kwa ushirikiano wa Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imejikita katika kuandaa na kufadhili miradi ya kimkakati kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi katika sekta kama nishati, uchukuzi, afya, elimu na TEHAMA.

Ameongeza kuwa Tanzania ilijiunga rasmi na Africa50 mwaka 2023 na tayari inanufaika kupitia maandalizi ya miradi mbalimbali ikiwemo Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini LNG, miundombinu ya usafirishaji wa umeme na huduma za dialysis.

Kaulimbiu ya mkutano huo ni “A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery,” ikiwa inaadhimisha miaka 10 ya Africa50 na kuangazia hatua za kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu Afrika. Mkutano huo pia utashuhudia utiaji saini wa makubaliano mbalimbali ya miradi ya maendeleo pamoja na ushiriki wa taasisi za umma na sekta binafsi.