Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima wa parachichi, hususan katika masuala ya bei na mfumo wa ununuzi, ili kuongeza kipato chao na kuimarisha sekta hiyo.
Hayo yamesemwa Agosti 2, 2026 na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Adam Salum, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale, mkoani Mbeya.
Salum amesema halmashauri inaendelea kuboresha uzalishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo kahawa, ambapo uzalishaji umefikia tani 34,000.
Amesema wataalamu wa kilimo wanaendelea kutoa ushauri kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya pembejeo na mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza kiwango cha mazao yanayokidhi daraja la kwanza.
“Kama wataalamu wa kilimo tunaendelea kuweka nguvu kwenye utoaji wa ushauri na matumizi sahihi ya pembejeo ili kupunguza mazao ya daraja la pili na kuongeza uzalishaji wa mazao ya daraja la kwanza kwa kiwango cha kutosha,” amesema.
Akizungumzia masoko ya parachichi, Salum amesema changamoto kubwa imekuwa ni uwepo wa madalali wanaowalaghai wakulima kwa kununua mazao kwa bei ya chini.

Amesema Serikali imeanzisha vituo vya kukusanyia parachichi ili kurahisisha biashara hiyo, huku Wilaya ya Rungwe ikiwa na vituo sita vinavyotumika kukusanya mazao hayo.
Aidha, amesema halmashauri inaendelea kutambua maeneo mengine ya kukusanyia mazao ili wakulima na wanunuzi wakutane sehemu moja na kufanya biashara kwa uwazi, hatua itakayosaidia kupunguza migogoro ya bei na ushawishi wa madalali.
“Kwa mfumo huu tunaamini wakulima watapata bei inayofanana, huku nafasi ya madalali wanaowalaghai ikipungua kwa kiwango kikubwa. Wilaya ya Rungwe pia ina kanda tatu za uzalishaji wa parachichi, jambo linalowezesha mavuno kufanyika kwa nyakati tofauti,” amesema.
Salum amesema pia halmashauri inaendelea kutafuta masoko mapya ya nje, ikiwemo soko la Afrika Kusini, ili kuongeza fursa za uuzaji wa parachichi la Rungwe.
Kwa upande wake, mkulima wa parachichi kutoka Kijiji cha Ntokela, Fodi Fungo, amesema changamoto kubwa ni madalali kuingilia bei licha ya Serikali kuweka bei elekezi.
“Madalali bado wanaendelea kupanga bei zao tofauti na bei elekezi ya Serikali. Pia bado kuna haja ya kuongeza elimu kwa wakulima ili wazalishe matunda yanayokidhi viwango vya masoko ya kitaifa na kimataifa,” amesema.
Naye mkulima mwingine, Brayson Bangula, amesema wakulima wameanza kujiunga katika vikundi ili kuimarisha uzalishaji na kupunguza utegemezi kwa madalali.
Amesema uzalishaji wa pamoja unarahisisha kupata wanunuzi wakubwa, huku wakulima pia wakianza hatua za kujenga kiwanda chao cha kuchakata parachichi ili kuongeza thamani ya zao hilo.
“Tukiwa pamoja tunazalisha kwa wingi na inakuwa rahisi kupata soko. Pia tayari tumeanza kujenga kiwanda chetu ili kuongeza thamani ya mazao yetu,” amesema.

More Stories
Millya:Ongezeni upatikanaji wa mbolea kwa ajili ya uzalishaji
TRA yaendelea kutoa elimu nane nane
WRRB Yapongezwa kwa Maandalizi ya Mnada wa Mifugo