Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma kuhusu misamaha na vivutio vya kodi vinavyopatikana katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wadau kuhusu fursa zinazosaidia kukuza uzalishaji.
Akizungumza katika maonesho hayo, Ofisa Mwandamizi wa Kodi wa TRA, Jackline Ntare, amesema mamlaka hiyo imeleta huduma mbalimbali ili kuwafikia wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na wananchi wengine kwa kuwapatia elimu ya kodi pamoja na huduma zinazotolewa na TRA.
“Banda la TRA linatoa huduma za usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), makadirio ya kodi kwa walipakodi wapya pamoja na elimu kuhusu mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotumika katika utoaji wa huduma za kodi”amesema
Ntare amesema wananchi wanaohitaji mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) wanapatiwa huduma kupitia mawakala waliopo katika banda hilo, huku wafanyabiashara wakipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mashine hizo.
Aidha, amesema TRA inaendelea kutoa elimu kuhusu mfumo wa Electronic Tax Stamp (ETS) kwa wazalishaji wa bidhaa, hususan vinywaji na bidhaa nyingine zinazotakiwa kutumia stempu za kielektroniki, ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria za kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Wakati huo huo, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TRA alisema alipata huduma ya usajili wa TIN kwa haraka baada ya awali kukumbana na changamoto za kimfumo wakati wa kufanya maombi.
Amesema alihudumiwa kwa muda mfupi na watumishi wa TRA na kueleza kuridhishwa na huduma aliyoipata, huku akiwahimiza wananchi wengine wenye mahitaji ya huduma za mamlaka hiyo kufika katika banda la TRA ili kupata msaada kwa wakati.

More Stories
Rungwe yaendelea kutatua changamoto za wakulima wa parachichi
WRRB Yapongezwa kwa Maandalizi ya Mnada wa Mifugo
DC Tabora, kigoma waitaka ewura ihamasishe wananchi