Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imesema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutategemea kwa kiwango kikubwa mafanikio ya sekta ya kilimo, hivyo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inapaswa kuelekeza uwekezaji wake katika maeneo ya kimkakati yatakayoongeza tija na ukuaji wa sekta hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar,jijini hapa leo Agosti 2,2026 alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa na Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha mtaji wa TADB kutoka Sh bilioni 60 hadi zaidi ya Sh bilioni 400 ili benki hiyo iweze kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na misitu ambazo ni nguzo muhimu za uchumi wa taifa.
Waziri Omar ameeleza kuwa Serikali inalenga kutumia maendeleo ya sekta hizo kupunguza umaskini, kuongeza kipato cha wananchi na kufikia lengo la uchumi wa dola trilioni moja kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, aliwataka viongozi wa Wizara ya Kilimo kuendelea kuwatafutia masoko wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini huku wakiongeza juhudi za kuwawezesha kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.
Pia aliipongeza wizara hiyo kwa kazi inayoendelea kufanya katika kuendeleza sekta ya kilimo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kuongeza tija, ajira, usalama wa chakula na kipato cha wananchi.


More Stories
WRRB Yapongezwa kwa Maandalizi ya Mnada wa Mifugo
DC Tabora, kigoma waitaka ewura ihamasishe wananchi
eGA yaimarisha kilimo kupitia Mifumo ya Kidigitali