August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa Shahiri waomba mbegu ziwafikie kwa wakati

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

BAADHI ya wakulima wa zao la Shahiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wameiomba Serikali na wadau wa kilimo kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika pamoja na upatikanaji wa mbegu kwa wakati, wakisema hatua hiyo itawaongezea ari ya kulima zao hilo kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mkulima wa Kijiji cha Muungano, Maiko Mbwilo, amesema hayo Agosti Mosi mwaka huu wakati akizungumza na Timesmajira Online, akieleza kuwa licha ya kuanza kulima shahiri mwaka jana, wakulima wengi bado wana mashaka kutokana na kutokuwa na uhakika wa bei na soko.

“Ili tuone faida ya zao hili, tunahitaji kwanza kuona bei nzuri na soko la uhakika. Tukijiridhisha na hilo, wakulima wengi watahamasika kulima shahiri kwa wingi zaidi,” amesema Mbwilo.

Amesema katika msimu wa mwaka 2025 walichelewa kuanza kilimo kutokana na mbegu kufika kwa kuchelewa, hali iliyosababisha baadhi ya mashamba kutofanya vizuri kwa kuwa zao la shahiri linahitaji kupandwa mapema na linategemea upatikanaji wa maji ya kutosha.

“Baadhi ya mashamba yaliyokuwa katika maeneo yenye mazingira mazuri yamefanya vizuri. Tunaamini tukipata mbegu mapema msimu ujao, uzalishaji utaongezeka na ubora wa mazao utakuwa wa kiwango cha juu,” ameongeza.

Mbwilo amesema changamoto kubwa iliyobaki ni soko la uhakika, akibainisha kuwa wakulima wengi wako tayari kuongeza uzalishaji endapo watapata uhakika wa wanunuzi.

Akizungumza katika viwanja vya Maonesho ya Wakulima Nanenane ya John Mwakangale jijini Mbeya, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka, amesema halmashauri imeanza kuhamasisha kilimo cha shahiri kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya Kiwanda cha Bia cha Serengeti.

Amesema kampuni hiyo imetoa mbegu bure kwa wakulima ili kuwahamasisha kuanza kulima zao hilo, huku ikiwa tayari kununua mazao yatakayozalishwa.

“Kiwanda cha Bia cha Serengeti kinahitaji tani nyingi za shahiri kama malighafi. Ndiyo maana kimetoa mbegu bure kwa wakulima wetu. Katika maonesho haya tumeweka shamba darasa kuonesha kuwa zao hili linastawi vizuri katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, na baadhi ya wakulima tayari wameanza kuvuna,” amesema Mwinuka.

Ameongeza kuwa hali ya ustawi wa shahiri ni nzuri na matarajio ni kuwa zao hilo litakuwa chanzo kipya cha kuongeza kipato kwa wakulima, akisisitiza kuwa lina soko la uhakika na halitofautiani sana na ngano katika uzalishaji.

Naye Bwana Shamba wa Kijiji cha Muungano, Lemi Jackson, amesema mafanikio ya kilimo cha shahiri yatategemea upatikanaji wa bei nzuri, soko la uhakika na mbegu kwa wakati.

Amesema wakulima wana hamasa ya kulima zao hilo, lakini wanahitaji kuhakikisha mazingira yote muhimu ya uzalishaji yanaboreshwa ili waweze kunufaika zaidi na kilimo hicho.