August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima Mbeya waiangukia Serikali kuhusu zao la shayiri

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya.

WAKULIMA wa zao la shayiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wameiomba Serikali na wadau wa kilimo kuhakikisha wanapata soko la uhakika, bei nzuri pamoja na mbegu kwa wakati, wakisema hatua hiyo itawaongezea ari ya kulima zao hilo kwa kiwango kikubwa.

Wakulima hao wameeleza hayo Agosti 1, 2026, katika mahojiano maalum na TimesMajira Online kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Mkulima wa Kijiji cha Muungano, Maiko Mbwilo, amesema licha ya baadhi ya wakulima kuanza kulima shayiri mwaka jana, wengi bado wana mashaka ya kuongeza uzalishaji kutokana na kutokuwa na uhakika wa bei na soko.

“Ili tuone faida ya zao hili, tunahitaji kwanza kuona bei nzuri na soko la uhakika. Tukijiridhisha na hilo, wakulima wengi watahamasika kulima shayiri kwa wingi zaidi,” amesema Mbwilo.

Amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025, walichelewa kuanza kilimo kutokana na mbegu kufika kwa kuchelewa, hali iliyosababisha baadhi ya mashamba kutofanya vizuri kwa kuwa zao hilo linahitaji kupandwa mapema na hutegemea upatikanaji wa maji ya kutosha.

Mbwilo amesema baadhi ya mashamba yaliyopo katika maeneo yenye mazingira mazuri yamefanya vizuri, akieleza kuwa upatikanaji wa mbegu mapema msimu ujao utaongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Cuthbert Mwinuka, amesema halmashauri imeanza kuhamasisha kilimo cha shayiri kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya Kiwanda cha Bia cha Serengeti.

Amesema kampuni hiyo imetoa mbegu bure kwa wakulima ili kuwahamasisha kuanza kulima zao hilo, huku ikiwa tayari kununua mazao yatakayozalishwa, na kuongeza kuwa shamba darasa lililoanzishwa kwenye maonesho hayo limeonesha kuwa shayiri inastawi vizuri katika wilaya hiyo.

Naye Bwana Shamba wa Kijiji cha Muungano, Lemi Jackson, amesema mafanikio ya kilimo cha shayiri yatategemea upatikanaji wa mbegu kwa wakati, bei nzuri na soko la uhakika, akisisitiza kuwa wakulima wana hamasa ya kuongeza uzalishaji endapo mazingira muhimu ya kilimo hicho yataboreshwa.