August 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Malisa: Serikali yaendelea kuimarisha sekta ya kilimo,uvuvi yafikia Bil.430

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Wakili Beno Malisa, amesema Serikali ina dhamira ya dhati, iliyo wazi na yenye matokeo katika kuendeleza sekta ya kilimo, huku bajeti ya Wizara ya Kilimo na Mifugo ikifikia Shilingi bilioni 430.

Amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti hiyo kila mwaka ili kuimarisha uzalishaji wa mazao na mifugo, huku akisisitiza kuwa wananchi wana wajibu wa kuisimamia Serikali ili kuhakikisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji inapungua.

Wakili Malisa alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

“Nazikumbusha halmashauri zote kuhakikisha zoezi la kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi linaendelea na linasimamiwa ipasavyo ili kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi,” alisema.

Aidha, alisema programu ya ruzuku ya mbolea na pembejeo imekuwa na manufaa makubwa kwa wakulima, na kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kila mkulima aweze kunufaika na fursa zinazotolewa.

Akizungumzia kilimo cha umwagiliaji, Wakili Malisa alisema Serikali imeendelea kupunguza utegemezi wa mvua kwa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 380 katika miradi ya umwagiliaji.

Alisema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inaendelea kunufaika na uwekezaji huo, akitaja Wilaya ya Mbarali kuwa miongoni mwa maeneo yanayoonyesha mafanikio makubwa kutokana na miradi ya umwagiliaji.

Atuganile John ni mkazi wa Mbalizi Jijini Mbeya amesema kuwa maonesho hayo ya wakulima yanaleta fursa kwa wakulima kujifunza vitu mbalimbali vinavyohusu kilimo pamoja jinsi ya kulima kilimo cha kisasa.

“Wapo baadhi ya wakulima wamekuwa na kilimo cha mazoea na wanahitaji upeo mkubwa wa kulima kilimo chenye tija kwao hivyo uwepo wa maonesho hayo kunawafanya kupanua wigo mpana wa kuongeza vitu kwenye kilimo chao”amesema.