Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
MAMLAKA ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewataka wananchi na wafanyabiashara kuhakikisha wanasajili majina wanayotumia katika shughuli zao za biashara ili kuzingatia matakwa ya sheria na kulinda biashara zao dhidi ya migogoro.
Akizungumza leo Agosti Mosi 2026 katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Usajili wa BRELA, Yusuf Mwasakafyuka, amesema sheria hairuhusu mtu kuendesha biashara kwa kutumia jina tofauti na jina lake binafsi bila kulisajili rasmi.
Mwasakafyuka amesema mfanyabiashara anayechagua kutumia jina maalumu, kama la saluni au duka, anatakiwa kulisajili ndani ya siku 28 tangu aanze kulitumia.
Ameeleza kuwa usajili huo unampa mmiliki haki ya kisheria ya kulitambua na kulilinda jina lake dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.
Aidha, amesema Msajili ana mamlaka ya kuchukua hatua kwa mtu anayekiuka utaratibu huo, ikiwemo kufuta usajili wa biashara husika, huku mhusika akiwajibika endapo matumizi ya jina hilo yatasababisha hasara kwa mmiliki halali.
Amehimiza wafanyabiashara kufuata taratibu zote za usajili wa majina ya biashara ili kujikinga na migogoro ya kisheria na kuhakikisha biashara zao zinapata ulinzi unaotambuliwa na sheria.

More Stories
Tusumuke Group yaonyesha teknolojia bora za kuku
Wanawake na vijana nguvu ya viwanda
FCC yawekeza kiwanda cha mbolea