August 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TVLA yaonya homa ya kutupa mimba mifugoni


Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WAKALA wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) umewataka wafugaji nchini kutumia chanjo ya homa ya kutupa mimba kwa mifugo ili kudhibiti ugonjwa huo unaosababisha hasara kubwa kiuchumi kwa wafugaji na kuhatarisha afya ya binadamu.


Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TVLA kwenye Maonyesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yaliyozinduliwa leo Agosti 1, 2026 na Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Daktari Mtafiti wa Magonjwa ya Mifugo wa TVLA, Issack Mengele, amesema ugonjwa huo umeenea katika mifumo mbalimbali ya ufugaji nchini, hususan kwa mifugo inayofugwa kwa mfumo wa malisho ya kuhamahama na ule wa kienyeji.


Amesema tafiti zinaonyesha maambukizi ni madogo kwa ng’ombe wa maziwa wanaofugwa ndani, lakini ni makubwa zaidi kwa mifugo inayofugwa katika jamii za wafugaji na wakulima, ambako pia matumizi ya maziwa yasiyochemshwa ni ya kawaida, hali inayoongeza hatari ya maambukizi kwa binadamu.


“Jamii nyingi za wafugaji na wakulima hutumia maziwa mabichi, hivyo zipo kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu,mara nyingi wagonjwa huchanganywa na wanaougua malaria au homa ya matumbo kwa sababu dalili zinafanana, hivyo hushindwa kupata matibabu sahihi kwa wakati,” alisema Mengele.


Ameeleza kuwa ugonjwa huo husababisha mimba kuharibika kwa mifugo, kupungua kwa uzalishaji wa maziwa, kupungua kwa idadi ya mifugo na hatimaye kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji kutokana na kushuka kwa uzalishaji na ukuaji wa mifugo.


Mengele amesema baadhi ya tafiti zimeonyesha maambukizi yanafikia kati ya asilimia 15 hadi 20 katika maeneo mengi, huku baadhi ya maeneo ya Arusha na Kanda ya Magharibi yakiripoti kiwango cha hadi asilimia 30 hadi 40, ingawa bado hakuna takwimu za kitaifa kutokana na tafiti kufanyika katika nyakati na maeneo tofauti.


Amesema Serikali kupitia TVLA tayari imeanza kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo, inayojulikana kama Brucella S19, ambayo inapendekezwa kutolewa kwa ndama jike kabla ya kuanza uzazi ili kuwakinga dhidi ya maambukizi na kupunguza athari za ugonjwa huo.


Amewahimiza wafugaji kujitokeza kupata huduma za chanjo na elimu ya afya ya mifugo, akieleza kuwa magonjwa yasiyoua mifugo kwa haraka ndiyo yanayosababisha hasara kubwa zaidi kwa sababu hupunguza uzalishaji na kudhoofisha uchumi wa wafugaji kwa muda mrefu.