Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa mchango wake katika kuwahudumia wakulima kupitia udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao pamoja na utoaji wa elimu ya matumizi salama ya viuatilifu.
Pongezi hizo amezitoa leo Agosti 1, 2026, alipotembelea banda la TPHPA wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 33 ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Dkt. Nchemba amesema utendaji wa TPHPA ni mfano mzuri wa utekelezaji wa kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka 2026 inayosema, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Aidha, aliielekeza TPHPA kuendelea kuboresha huduma zake na kuzifikisha kwa wakulima wengi zaidi nchini ili kulinda mazao dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu, kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha usalama wa chakula.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, alimweleza Waziri Mkuu kuwa Mamlaka hiyo imeimarisha jitihada za kudhibiti baa la njaa kwa kulinda afya ya mimea, kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya viuatilifu na kuimarisha huduma za afya ya mimea ili kuongeza tija kwa wakulima.
Profesa Ndunguru alisema hatua hizo zimewezesha wakulima kupata huduma bora zinazochangia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

More Stories
Waziri Mkuu Aipongeza TAFICO kwa mafanikio Nanenane
Mwigulu ataka huduma za TPHPA ziwafikie wakulima wengi
Mwigulu:TADB ni muhimu kuongeza uzalishaji wa kilimo