Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Bayport Financial Services Tanzania imeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa kompyuta 20 aina ya HP na mashine mbili za kuchapisha na kunakili (All-in-One Printers) zenye thamani ya jumla ya TZS milioni 100 kwa Idara ya Elimu ya Jimbo la Kibamba, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza dhamira yake ya kusaidia sekta ya elimu na maendeleo ya taifa.
Makabidhiano hayo yamefanyika rasmi katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Anazaki, Kimara, na kuhudhuriwa na Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, pamoja na viongozi wa wilaya, maafisa wa elimu, wanahabari na wawakilishi wa Bayport.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Idara ya Mikopo Bayport Financial Services Tanzania, Amina Amani, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya juhudi za kampuni kuacha alama ya kudumu katika jamii wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuhudumia Watanzania.
“Tulipotafakari namna bora ya kuadhimisha hatua hii muhimu, tulijiuliza ni kwa namna gani tunaweza kuacha urithi ambao utaendelea kuleta mabadiliko hata baada ya maadhimisho haya kuisha. Jibu lilikuwa wazi; tulitaka kufanya uwekezaji ambao utaendelea kuleta thamani kwa jamii na kuchangia safari ya maendeleo ya Tanzania kwa miaka mingi ijayo,”amesema Amani.
Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Bayport imehudumia zaidi ya Watanzania 430,439, wengi wao wakiwa watumishi wa umma, na kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni 529, iliyowasaidia wateja wake kutimiza malengo yao ya kifedha na maendeleo binafsi.
Kompyuta na mashine za uchapishaji zilizotolewa zinatarajiwa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa elimu kwa njia ya kidijitali katika Jimbo la Kibamba kwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na kuongeza upatikanaji wa teknolojia kwa maafisa wa elimu.
“Kompyuta hizi ni zaidi ya vifaa vya teknolojia; ni fursa. Zitawawezesha maafisa wa elimu na walimu wanaojenga mustakabali wa taifa letu huku zikichangia kuboresha utoaji wa huduma kupitia mageuzi ya kidijitali,” ameongeza Amani.
Bayport imeeleza kuwa wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza ajenda yake ya mageuzi ya kidijitali, upatikanaji wa teknolojia za kisasa ni muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za umma na kuandaa vizazi vijavyo kufanikiwa Katika uchumi wa kidijitali.
Kampuni hiyo imesisitiza kuwa mchango huo unaonesha dhamira yake ya kuwa taasisi inayowajibika kwa jamii na mshirika hai katika maendeleo ya taifa, mbali na jukumu lake la kutoa huduma za kifedha.

Bayport pia imetoa shukrani kwa wateja wake, hususan watumishi wa umma wa Tanzania, ambao imani na ushirikiano wao vimewezesha ukuaji na mafanikio ya kampuni hiyo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Mchango huu ni sehemu ya mpango wa Bayport wa Uwekezaji kwa Jamii (Corporate Social Investment) Katika maadhimisho ya miaka 20, unaolenga kuleta matokeo endelevu katika jamii zinazohudumiwa na kampuni hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo vya TEHAMA, Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angellah Jasmine Kairuki ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibamba Mbunge wa Jimbo la Kibamba amesema kuwa msaada huo wa vifaa vya TEHAMA ni utekelezaji wa mkakati wa kuifanya Kibamba kuwa jimbo la kidijitali (Make Kibamba Digital) umeanza rasmi kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Vifaa hivi vimekuja muda muafaka kwani vitarahisisha usimamizi wa elimu, mawasiliano kati ya idara mbalimbali, uratibu wa mitihani na utoaji wa huduma kwa walimu, wazazi na wanafunzi.
“Tunaanza na idara za elimu, lakini huu ni mpango mpana wa kuifanya Kibamba kuwa jimbo la kidijitali. Tutaendelea kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za sekondari, ofisi za kata na maeneo mengine ya huduma za umma kwa awamu,”amesema Kairuki.
Amebainisha kuwa tayari maandalizi yamekamilika kuzipatia shule za sekondari vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta, projectors na vifaa vingine vya kisasa, akisisitiza kuwa utekelezaji huo utafanyika hatua kwa hatua ndani ya kipindi cha miaka mitatu hadi minne.
Aidha, ametoa shukrani kwa Bayport Financial, pamoja na Idara ya Elimu ya Manispaa ya Ubungo kwa ushirikiano wao, akisema Bayport itaendelea kushirikiana na Serikali na jamii katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.

More Stories
Onyo kali latolewa dhidi ya Utoroshaji wa Dhahabu Kahama
Mama Ongea na mwanao kufanya Dua maalumu kwa wasanii waliopita
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ashiriki uzinduzi wa boti mpya za doria