Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Serikali itaharakisha kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Uchukuzi ili kuimarisha taaluma hiyo, kuongeza ubora wa huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi nchini.
Akifungua Kongamano la Wataalamu wa Usafirishaji na Lojistiki lililofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Waziri Mkuu amesema Serikali pia itafanyia kazi mapendekezo ya kuanzisha vitengo vya usimamizi wa usafirishaji katika taasisi za umma na halmashauri ili kuboresha matumizi ya rasilimali za Serikali.

Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara ya Uchukuzi huku akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA) katika kuendeleza taaluma hiyo, akieleza kuwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unahitaji wataalamu wenye ujuzi na weledi wa hali ya juu.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema chuo kitaendelea kuzalisha wataalamu mahiri wa usafirishaji na lojistiki watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Mwenyekiti wa TALTA,Alphonce Mwingira, amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuhimiza kuanzishwa kwa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji, hatua itakayoongeza hadhi ya taaluma na kuimarisha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkoa huo utaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji na lojistiki ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Waziri Mkuu amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali imezipokea hoja zote zilizowasilishwa na washiriki wa kongamano na itazifanyia kazi kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika, akieleza kuwa sekta imara ya uchukuzi ni msingi muhimu wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

More Stories
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ashiriki uzinduzi wa boti mpya za doria
Twange awataka wanasheria wa Tanesco kusimamia Maadili na Taaluma
Mchange ahoji Dkt.Nchimbi anajua madhara ya kauli zake