Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) na Kaimu Meneja wa Huduma za Kiswahili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), Mgaya Kingoba, amesema uhuru wa kutoa maoni una mipaka ya kisheria na kimaadili, hivyo haupaswi kutumiwa kutoa matusi, kudhalilisha wengine, kuchochea chuki au kusambaza taarifa zisizo sahihi.
Kingoba amesema hayo leo, Julai 30, 2026, alipowasilisha mada kuhusu “Kuimarisha Uzalendo katika Uandishi wa Habari ili Kulinda Amani, Umoja na Mshikamano” katika siku ya pili ya mafunzo kwa watumishi wa Bongo FM, redio dada ya TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania), yaliyofanyika katika Ofisi za JAB jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 29, 2026.
Amesema ukosoaji ni sehemu muhimu ya uhuru wa kujieleza, lakini unapaswa kulenga kuonesha kasoro na kuchochea maboresho badala ya kushambulia watu, kutumia lugha ya kejeli au kubomoa imani ya jamii kwa taasisi.
“Mkosoaji mzalendo hafichi makosa, lakini pia hatumii matusi, kejeli au upotoshaji. Anakosoa kwa ukweli, ushahidi na lugha ya staha, akiwa na lengo la kujenga na kuboresha,” amesema Kingoba.

Ameeleza kuwa mkosoaji mzalendo hujenga ukosoaji wake katika misingi ya ukweli, ushahidi, muktadha, lugha ya staha, maslahi ya umma na mapendekezo ya suluhisho.
Aidha, amewataka watangazaji kutambua kuwa uhuru wa kujieleza hauondoi wajibu wao wa kulinda utu wa watu, amani na mshikamano wa kitaifa.

Kingoba amesema uzalendo katika utangazaji hauishii katika kuipenda nchi kwa maneno, bali unapaswa kuonekana katika maamuzi ya kitaaluma yanayolinda ukweli, umoja, amani na maslahi ya Taifa na kwamba uchaguzi wa maneno na namna ya kuendesha mijadala ya moja kwa moja unaweza kujenga jamii au kusababisha migawanyiko.
Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria hiyo inatambua uhuru wa Waandishi wa Habari na vyombo vya habari katika kutafuta, kuhariri, kuchapisha na kutangaza habari, lakini inaweka pia wajibu wa kuzingatia sheria, maadili, weledi na haki za wengine.

Amesema uhuru wa habari na uwajibikaji vinapaswa kwenda pamoja ili kulinda taaluma, maslahi ya jamii na Taifa.
Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi wa habari, uzalendo na wajibu wa watangazaji katika kutumia uhuru wa kujieleza kwa weledi na uwajibikaji.

More Stories
Wanne wakamatwa kwa mauaji ya Mwalimu Dimoso
Mawakili wa Serikali wanolewa kuhusu sheria ya Fedha
Yegella:Zimamoto nguzo ya ustawi Mbeya