
-Pia Ng’ombe 135 za watuhumiwa wanaotafutwa nazo zinashikiliwa.
Na Moses Ng’wat, Songwe.
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya Mwalimu wa Shule ya Sekondari Galula, Nisetasi Dimoso (43), huku ng’ombe 135 wanaodaiwa kumilikiwa na watuhumiwa wengine wanaotafutwa wakishikiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 30, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Alfqjiri ya Julai 30, 2026, katika Kitongoji cha Swela, Kijiji cha Ifuko, Kata ya Chang’ombe, Wilaya na Mkoa wa Songwe.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwiguku Luhende (21), Boniface Mwawa (20), Masanja Kishiwa, maarufu Kasamweli (30), na Luhende Melani (19), wote wakazi wa Kitongoji cha Swela.
Kwa mujibu wa Senga, Dimoso alishambuliwa usiku wa Julai 26, mwaka huu, baada ya kuwazuia watu waliodaiwa kuwa wafugaji kupitisha mifugo katikati ya eneo la Shule ya Sekondari Galula.
Inadaiwa kuwa baada ya kuzuiwa, mmoja wa vijana waliokuwa wakipitisha mifugo aliwaita watu wengine wanaodaiwa kuwa wamiliki wa mifugo hiyo, ambao walifika na kumshambulia mwalimu huyo kabla ya kutoweka.
Baada ya shambulio hilo, Dimoso alipelekwa Kituo cha Afya Mbuyuni kwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, ambako alifariki dunia Julai 28, mwaka huu, akiwa anaendelea na matibabu.
Senga amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo.
Aidha, Senga amesema Ng’ombe 135 wanaodaiwa kumilikiwa na baadhi ya watuhumiwa wanaotafutwa walikutwa wakiwa wamelekezwa porini na sasa wanashikiliwa na uongozi wa Kijiji cha Ifuko.
“Watuhumiwa wengine ambao majina yao tunayafahamu na tunaendelea kuwatafuta, ng’ombe wao 135 wanashikiliwa na uongozi wa Kijiji cha Ifuko,” amesema Senga.

More Stories
Kingoba:Uhuru wa kutoa maoni uende sambamba na uwajibikaji
Mawakili wa Serikali wanolewa kuhusu sheria ya Fedha
Yegella:Zimamoto nguzo ya ustawi Mbeya