Na Mwandishi wetu,Timesmajira
MWANDISHI Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amefungua mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali kuhusu Sheria ya Fedha (Finance Act), yakilenga kuwaongezea uwezo wa kitaalamu katika uandaaji na utekelezaji wa sheria hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa njia ya mtandao yamewakutanisha Mawakili wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini, yakiratibiwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria. Mafunzo hayo yanaendeshwa na wakufunzi kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na Wizara ya Fedha.
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Njole alisema Sheria ya Fedha ni mhimili mkuu wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, hivyo Mawakili wa Serikali wana mchango mkubwa katika kuchambua, kuandika, na kuhakikisha vifungu vyake vinakidhi mahitaji ya kisheria na kiuchumi.

“Mafunzo haya yanalenga kuwawezesha Mawakili wa Serikali kufahamu nafasi yao katika mchakato mzima wa uandaaji na ukamilishaji wa Sheria ya Fedha, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,” amesema.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kiufundi kuhusu mabadiliko mbalimbali ya kodi na masuala ya fedha yanayofanyika kila mwaka kupitia Sheria ya Fedha, pamoja na kuongeza ufanisi katika uandishi wa muswada wa sheria hiyo.
Njole amesema washiriki pia watapata fursa ya kujadili kwa kina nafasi ya Mawakili wa Serikali katika mchakato wa utungaji wa Sheria ya Fedha na kupata uelewa wa mfumo wa kisheria unaosimamia utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali.

“Kupitia mafunzo haya tutapata uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa Mawakili wa Serikali katika utungaji na utekelezaji wa Sheria ya Fedha, jambo litakaloongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu,”amesema.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kuelewa kwa undani sababu na malengo ya marekebisho mbalimbali yanayofanywa katika Sheria ya Fedha kila mwaka, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kutoa mchango katika kuboresha mfumo wa sheria na usimamizi wa fedha za umma.


More Stories
Kingoba:Uhuru wa kutoa maoni uende sambamba na uwajibikaji
Yegella:Zimamoto nguzo ya ustawi Mbeya
Katambi akerwa BOQ kukosekana kwenye miradi