July 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yegella:Zimamoto nguzo ya ustawi Mbeya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, amesema ukuaji wa kasi wa Halmashauri hiyo unaifanya huduma ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa nguzo muhimu katika kulinda maisha na mali za wananchi, sambamba na kuimarisha ustawi wa jamii.

Yegella amesema hayo Julai 29, 2026, alipokutana na maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kueleza shughuli wanazozitekeleza baada ya kuanza kutoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Amesema kuanzishwa kwa kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji karibu na wananchi kutarahisisha mwitikio katika matukio ya dharura na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na majanga ya moto.

Amesema awali huduma hizo zilikuwa zikitolewa kutoka Jiji la Mbeya, hali iliyoweza kuongeza muda wa kufika katika maeneo ya matukio.

“Ninamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa kutusogezea huduma za Jeshi la Zimamoto katika halmashauri yetu. Hii ni hatua muhimu ambayo itanufaisha wananchi na kuongeza usalama katika eneo letu,” amesema Yegella.

Ameongeza kuwa uwepo wa kituo hicho utasaidia kufikisha huduma kwa wakati, kulinda miundombinu na mali za wananchi, huku halmashauri ikiendelea kukua na kupanuka kwa kasi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kilichopo katika Makao Makuu ya Halmashauri, Iwindi, S/SGT Leah Mwanyambo, amesema kituo hicho kinahudumia wananchi wa Mbalizi na maeneo mengine ya wilaya kwa ufanisi zaidi.

Amesema tangu huduma hizo zianze kutolewa katika eneo hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanikiwa kudhibiti matukio mawili ya moto yaliyohusisha majengo na kuzuia madhara makubwa yaliyoweza kujitokeza.

Mwanyambo amewahimiza wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya majanga ya moto kwa kupiga namba ya dharura 114, pamoja na kushiriki katika mafunzo ya kinga na usalama yanayotolewa na jeshi hilo.

Naye mkazi wa Mbalizi, Suzana Antony, amesema ujio wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni faraja kwa wananchi kutokana na matarajio ya kupungua kwa muda wa kufika kwenye maeneo ya matukio na kuongezeka kwa uwezekano wa kuokoa maisha na mali.