July 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katambi akerwa BOQ kukosekana kwenye miradi

Na Moses Ng’wat, Mbozi.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amekerwa na kutokuwepo kwa Hati ya makadirio ya gharama za ujenzi (BOQ) kwenye maeneo ya miradi, akisisitiza kuwa nyaraka hiyo ni muhimu katika kuwezesha ukaguzi na uhakiki wa thamani ya fedha zinazotumika.

Hatua hiyo imekuja baada ya mkandarasi anayetekeleza mradi wa kuboresha na kupanua huduma ya maji Vwawa–Mlowo, wilayani Mbozi, kushindwa kuwasilisha BOQ wakati Waziri alipofanya ukaguzi wa mradi huo Julai 30, 2026.

Katambi amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anawasilisha BOQ hiyo kabla ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe, akisema hataki kuona anafika kwenye miradi inayotekelezwa bila kuwepo nyaraka hizo muhimu.

Amesema katika ziara yake, kila mradi atakaokwenda kuukagua lazima uwe na BOQ eneo la utekelezaji ili kumwezesha yeye na viongozi wengine kuhakiki viwango vya kazi, vifaa vinavyotumika na thamani halisi ya fedha zilizotengwa.

“Napaswa kila ninapofika kwenye mradi nikute na nione BOQ ili nijue kiwango cha kazi na thamani ya fedha zinazotumika, kwa sababu Rais anajitahidi kukusanya kodi ili wananchi wapate huduma,” amesema Katambi.

Amesema BOQ lazima iwe sahihi na ipatikane eneo la mradi ili iwe rahisi kwa viongozi kufanya uhakiki wa kazi zinazotekelezwa, huku akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kudhibiti matumizi yasiyoendana na makubaliano ya kimkataba.

Akizungumza mbele ya Waziri Katambi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vwawa–Mlowo (VWAMWASSA), Clavery Casmir, amesema mradi huo umefikia asilimia 32 ya utekelezaji na unatarajiwa kupunguza kiwango cha maji yasiyolipiwa kutoka asilimia 38 hadi asilimia 34.

Amesema mradi huo unalenga kunufaisha wakazi 29,811, kupunguza upotevu wa zaidi ya lita 500,000 za maji kwa siku na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma baada ya kukamilika.

Casmir amesema mradi huo unahusisha kubadilisha mtandao chakavu wa maji, kufunga mita janja na kuboresha mfumo wa usambazaji, huku kukamilika kwake kukitarajiwa kuboresha huduma katika maeneo ya Ilembo, Ilolo, Mwenge, Vwawa Day, Old Vwawa, Ichenjezya na Isangu.