July 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB yajivunia kuongeza mtaji hadi bil.452.16/-

Na Zena Mohamed ,Timesmajiraonline,Dodoma

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kufadhili sekta ya kilimo baada ya mtaji wake kuongezeka kutoka shilingi bilioni 60 hadi shilingi bilioni 452.16, hatua iliyotokana na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo  Julai 30, 2026, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB), Frank Nyabundege, kuhusu utekelezaji wa benki hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27 amesema kuwa ongezeko hilo la mtaji limeiwezesha benki kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi kupitia huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga kuongeza tija na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Nyabundege amesema  Serikali iliongeza mtaji wa benki kwa awamu tofauti, ikiwemo shilingi bilioni 208 mwaka 2021, shilingi bilioni 174.16 mwaka 2024 kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), pamoja na shilingi bilioni 10 mwaka 2025, hatua zilizoongeza uwezo wa TADB kutekeleza majukumu yake ya maendeleo.

Alieleza kuwa mbali na mtaji wa Serikali, TADB imefanikiwa kuvutia mikopo na fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo, ikiwemo AFD, JICA na IFAD, jambo lililochangia kuimarisha uwezo wa benki kufadhili miradi ya kilimo na kuendeleza diplomasia ya uchumi kupitia uwekezaji katika sekta hiyo.

“Takwimu  zinaonesha kuwa asilimia 73.6 ya mikopo yote iliyotolewa na benki katika kipindi cha miaka mitano ilitolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, hali inayoonesha  kuongezeka kwa kasi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo wakati wa Serikali ya Awamu ya Sita,”amesema.

Alisema kuwa  kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, TADB imejipanga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kukuza matumizi ya teknolojia, kuimarisha minyororo ya thamani na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika biashara za kilimo.

Aidha, benki itaendelea kufadhili miradi inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuongeza ushirikiano na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo, huku ikichochea uongezaji thamani wa mazao na kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Nyabundege alisema TADB itaendelea kuwa mshirika mkuu wa maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kuchangia usalama wa chakula, ajira na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Pia aliwataka wananchi kutembelea banda la benki katika Maonesho ya 88 ya Kimataifa ya Biashara ya Kilimo (Nane Nane), ambapo TADB ni Mdhamini Mkuu wa maonesho hayo mwaka 2026, ili kujionea huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na benki.