Na Mwandishi wetu Arusha
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Tanga imeibuka miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri zaidi nchini katika usimamizi wa ununuzi wa umma baada ya kutwaa tuzo mbili katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma la mwaka 2026 linaloendelea jijini Arusha.
Tuzo hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinatokana na mafanikio ya TARURA Tanga katika kuzingatia kikamilifu matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na kuonyesha ufanisi mkubwa katika utoaji wa mikataba.
Katika tuzo ya kwanza TARURA Tanga ilitambuliwa kwa kutekeleza kwa kiwango cha juu matakwa ya sheria yanayotaka asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kutengwa kwa ajili ya vikundi vya kijamii hatua iliyotajwa kuwa mfano bora wa utekelezaji wa sera za Serikali za kuwainua makundi yenye mahitaji maalum kiuchumi.
Tuzo ya pili ilitokana na mafanikio ya Wakala huo katika usimamizi wa mikataba baada ya kufanikisha utoaji wa mikataba 106 katika mwaka wa fedha 2025/2026, jambo lililoiweka miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri zaidi nchini.
Mafanikio hayo yanaendelea kuithibitisha TARURA kuwa miongoni mwa taasisi zinazosimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha za umma kupitia uzingatiaji wa sheria, uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ununuzi nchini.

More Stories
PPAA yashiriki kongamano la 10 Ununuzi,yawaita wadau
Sangu :Wadau tuchangie madawati
ACT Wazalendo yaitaka SMZ kutoa ufafanuzi wa gharama za miundombinu ya AFCON 2027