July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kukataa dawa za kulevya kwa dhati

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Sixtus Mapunda amewataka wananchi kukataa matumizi na biashara ya dawa za kulevya kutoka moyoni sio mdomoni.

Amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya tatizo hilo hayawezi kufanikiwa ikiwa jamii itapinga dawa hizo kwa maneno pekee.

Mapunda amayasema hayo leo katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke alipokuwa akifungua Tamasha la kuifikia na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Amesema, juhudi zinazofanywa na DCEA chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo kukabiliana na usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini zinastahili kuungwa mkono na jamii nzima.

Hata hivyo amempongeza Kamishna Jenerali Lyimo kwa jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Amesema, jamii ni hatua muhimu katika kuongeza uelewa wa programu ya kuifikia na kuhamasisha wananchi na kuwahusisha moja kwa moja katika kutokomeza tatizo hilo.

“Jiografia ya Wilaya ya Temeke inafanya suala la matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya kuwa changamoto inayohitaji ushirikiano wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi,” amesema Mapunda

Amesema, elimu inayotolewa na DCEA itasaidia wananchi kutambua madhara ya dawa za kulevya mapema, kuzungumza na watoto kuhusu hatari zake, kukataa vishawishi vya matumizi na kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa hizo.

Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kuwajengea uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Pia, amesema jamii inapaswa kuwa makini na vishawishi vinavyoweza kuwafanya vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na tamaa ya maisha ya anasa yanayoonyeshwa kupitia mitandao ya kijamii bila kuelewa chanzo cha utajiri huo.

Mkuu huyo wa wilaya, amesisitiza pia umuhimu wa kuendelea kuvunja mitandao ya usambazaji wa dawa za kulevya, akisema wahusika katika biashara hiyo wamekuwa wakisababisha madhara makubwa kwa wananchi, hususan vijana na watu wenye kipato cha chini.

“Ndugu zangu wa Temeke, tukatae dawa za kulevya moyoni, siyo mdomoni. Kwani mkiendelea kukataa mdomoni badala ya moyoni, hii vita inakuwa ngumu,” amesema.

Amesema,dawa za kulevya ni tishio kwa usalama wa Taifa kwa kuwa zinadhoofisha nguvu kazi, kuharibu maisha ya vijana, kuongeza uhalifu na kuathiri ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Kamishna Msaidizi wa Tiba na Huduma za Utengamao wa Mamlaka hiyo, Dkt. Cassian Nyandindi amesema, tatizo la dawa za kulevya linahitaji jitihada shirikishi kutoka kwa Serikali, taasisi, familia na jamii kwa ujumla.

Ameesema, DCEA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inafikia

Dkt. Nyandindi amesema, tamasha hilo ni sehemu ya jitihada za kuwaleta wananchi pamoja, kuwaelimisha na kuwahamasisha kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Amesema, tatizo hilo haliwezi kumuacha mtu yeyote salama, kwa kuwa hata kama mtu halimgusi moja kwa moja, linaweza kuathiri ndugu, jamaa, marafiki au jamii inayomzunguka.

Ametoa wito kwa wananchi kote nchini kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika, kuelimisha jamii na kukataa kwa vitendo matumizi na biashara ya dawa hizo.

i