Na Mwandishi Wetu, Lushoto
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa sh. bilioni 6.4 kwa ajili ya ukarabati wa Soko Kuu na Stendi Kuu ya Mabasi Lushoto mjini.
Ameyasema hayo Julai 22, 2026 kwenye hafla fupi ya utiaji sahihi wa mikataba ya miradi ya uboreshaji wa ujenzi wa Soko Kuu la mjini Lushoto na ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi, na Msimamizi Mshauri wa Miradi ya ujenzi na uboreshaji wa soko pamoja na ujenzi wa stendi ya mabasi iliyofanyika pembezoni mwa soko hilo.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia sisi wana Lushoto tuweze kupata sh. bilioni 6.4 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya ya Soko la Lushoto pamoja na ujenzi wa stendi mpya ya Lushoto. Niushukuru sana uongozi wa Mkoa na Tanga na ule wa Wilaya ya Lushoto kwa kazi kubwa mliyoifanya.
“Nilikuwa nafuatilia mnavyoambiana tuweze kuondoka hapa ili muweze kuruhusu ujenzi wa miundombinu hii ifanyike. Ninafahamu kulikuwa na tatizo kidogo, na kulikuwa na shida kidogo. Lakini ndugu zangu naomba niwaambie, tunapoona tunakwenda kufanya jambo lolote la maendeleo kuna athari zinaweza kutokea. Ni kama vile barabara inapotengenezwa kunakuwa na vumbi, lakini baada ya barabara kukamilika kila mtu anafura” amesema Profesa Shemdoe.
Profesa Shemdoe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto, amesema Mji wa Lushoto ni wa kitalii, hivyo lazima upendeze ili kuwavutia wageni, lakini pia Wilaya ya Lushoto ni kongwe, na historia ya kuanzishwa vitu vingi vya kitaifa ikiwemo kuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini, Ikulu ya Magamba ambayo walikuwa wanaishi Magavana wa Kijerumani na Kingereza, hivyo kuwepo na soko la kisasa na stendi ya kisasa, itafanya wafanane na miji mingine nchini.

Profesa Shemdoe amewahakikishia wafanyabiashara kuwa watarudi kwenye soko hilo baada ya mwaka mmoja, kwani ujenzi wake unaanza Agosti 3, 2026, na utakamilika Agosti 2, 2026. Na watarudi hapo kukiwa bora zaidi na wataendelea kujitafutia riziki kama kawaida, huku akiwakumbusha wananchi kuwa fedha hizo sh. bilioni 6.4 hazikwenda kama Upepo wa Kisulisuli, bali zimepiganiwa hadi kufika Lushoto.
Akisoma taarifa ya miradi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Dkt. Ikupa Mwasyoge amesema Mradi wa Uboreshaji na Ujenzi wa miundombinu ya Soko pamoja na ujenzi wa Stendi ni miradi ambayo inatekelezwa chini ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini pia inaendana na Dira ya Maendeleo ya 2020/2050 inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji, huduma za biashara na masoko.
“Leo tunategemea kusaini mikataba ya miradi ya soko, stendi na msimamizi mshauri yenye thamani ya jumla ya sh. 6,276,351,120 kama ifuatavyo. Sh. 4,239,823,534 (pamoja na VAT) ambayo ni fedha kwa ajili ya ukarabati wa soko lililopo na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo maduka, vyoo, vizimba na maeneo ya maegesho ya magari. na Jumaja Contractors Company Limited.

“Aidha, Mradi wa Ujenzi wa Stendi Mpya wenye thamani ya sh. 1,845,367,586 (pamoja na VAT) ambayo ni fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Stendi, maduka, vyoo, pamoja na eneo la maegesho ya magari madogo. Mkandarasi tutakayesaini naye mkataba kwa thamani hiyo ya fedha ni Bandiko Construction Limited. Na kazi ya Mkandarasi mshauri wa kusimamia miradi yote miwili yenye thamani ya sh. 191,160,000 (pamoja na VAT) na Volumetric Arch Consult LTD” amesema Dkt. Ikupa.
Dkt. Ikupa amesema wao kama Halmashauri, wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt. Samia kwa kuwapatia miradi hiyo muhimu kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Lushoto. Pili, wamemshukuru Profesa Shemdoe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kwa kuendelea kupigania maendeleo ya jimbo hilo na kuifanya Lushoto izidi kupiga hatua kimaendeleo.

Wakati huo huo, Profesa Shemdoe pia amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa miradi mingine mingi kwenye Jimbo la Lushoto ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya na shule ya msingi vinavyojengwa Kata ya Gare. Kata ya Makanya kunajengwa Kituo cha Afya sambamba na ukarabati wa barabara ya Mlola hadi Makanya. Barabara ya Malibwi- Kwekanga- Kilole- Ngwelo inajengwa.
“Ukifika Kata ya Magamba kuna Shule ya Sekondari Shukilai. Kuna fedha sh. milioni 528 zimewekwa pale. Kata ya Kwemashai kuna nyumba za walimu zinajengwa, Kata ya Ubiri kunajengwa madarasa, ukifika Kata ya Mbwei kuna daraja lilishindikana miaka nenda rudi, leo hii ukifika, Mkandarasi anafanya kazi” amesema Profesa Shemdoe.
Profesa Shemdoe amesema kilio cha wananchi wa Tarafa za Mlola na Mlalo kimesikilizwa, na sasa barabara ya kutoka Magamba- Migambo- Malibwi- Mbwei- Mlola, na ile ya kutoka Magamba- Lukozi- Malindi- Mlalo ambazo ni za Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) zinakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami, na sasa hivi amepatikana Mshauri ambaye anakwenda kuzifanyia Upembuzi Yakinifu.

Barabara ya kutoka Lushoto hadi Mlola yenye kilomita 44, na ile ya kutoka Magamba hadi Mlalo kilomita 44 zimekuwa zinajengwa kidogo kidogo kwa kiwango cha lami, ambapo kwa mwaka zinajengwa kila moja kwa kilomita moja hadi tatu kwa mwaka, na barabara ya Lushoto- Mlola imefika Kata ya Migambo, huku ile ya Lushoto- Mlalo imefika Kata ya Magamba.




More Stories
BRELA yarahisisha usajili wa haki ya dhamana Kidijitali
Sangu: Tanzania kushiriki maonesho ya 26 ya Wajasiliamali Kigali
Taasisi za umma zatakiwa kuachana na utendaji wa mazoea ili kufanikisha Dira 2050