November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tasnia ya ukuzaji viumbe maji yakua nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Njombe

KWA kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2019/2020, tasnia ya Ukuzaji Viumbe Maji imekua ambapo idadi ya mabwawa ya samaki imeongezeka kutoka 22,545 hadi 26,445 na vizimba kutoka 109 hadi 431.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah, kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa yanayofanyika mkoani Njombe.

Amesema wastani wa ulaji wa samaki kwa mtu kwa mwaka hapa nchini umeongezeka kutoka kilo 8.2 mwaka 2018/2019 hadi kufikia kilo 8.5 mwaka 2019/2020.

Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, ulaji samaki duniani ni kilo 20.3 kwa mtu kwa mwaka (FAO, 2018).

“Sekta ya Mifugo inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia lishe bora ambayo inawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kukuza pato la Taifa.

Sekta hii ina mchango mkubwa katika kuwapatia wananchi ajira, chakula, lishe, kipato na fedha za kigeni. Katika mwaka 2019/2020, Sekta ya Mifugo ilichangia asilimia 7.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2018/2019.

Pia, Sekta ya Mifugo imekua kwa asilimia tano kwa mwaka 2019/2020 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019,” amesema Dkt. Tamatamah.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 uzalishaji wa maziwa umefikia lita bilioni 3.0 ukilinganisha na lita bilioni 2.7 zilizozalishwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

Alifafanua kwamba ongezeko la uzalishaji limetokana na ongezeko la ngÂ’ombe na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini.

Aidha, amesema uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kufikia tani 701,679.1 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 tofauti na tani 690,629 zilizozalishwa mwaka 2018/2019.

Aidha, pamoja na ongezeko hilo, bado ulaji wa nyama na maziwa nchini sio wa kuridhisha, hivyo, niendelee kutoa rai kwa wananchi kuongeza ulaji wa nyama ili tuweze kufikia kiwango kilichosimikwa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) cha kilo hamsini kwa mwaka kwa mtu mmoja na unywaji wa maziwa kufikia lita 200 kwa mtu kwa mwaka.

Pia amesema uzalishaji wa mayai uliongezeka nchini kutoka mayai bilioni 3.58 mwaka 2018/2019 hadi bilioni 4.05 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 13.3.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt.Rashid Tamatamah (kulia) akifafanua jambo kwenye banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi baada ya Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula duniani ambaye pia Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba (kushoto) kufika katika banda hilo juzi.

Kwa mujibu wa Dkt. Tamatamah, pamoja na ongezeko hilo aliwasihi wafugaji na wakulima kuendelea kujifunza teknolojia mbalimbali zinazooneshwa kwenye maadhimisho hayo.

“Ongezeko hili la mazao ya mifugo na uvuvi limetokana na dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na tatizo la uhaba wa chakula nchini hususan katika suala la upatikanaji wa protini ya samaki na nyama,” amesema.

Aliongeza kwamba ongezeko hilo limetokana na chachu ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.

“Madhimisho hutukumbusha kwa dhati kabisa kila mwaka umuhimu wa kuwatendea haki Watanzania kwa kuhakikisha kuwa chakula cha kutosha kinapatikana, na chenye ubora stahiki na kila mmoja kuhakikisha kuwa kinalindwa ili kisiharibike kabla au baada ya kuvunwa na hatimaye kuliwa,” amesema.

Aliwakumbusha wafugaji na wavuvi kuacha kuzalisha kwa mazoea, badala yake watumie tekinolojia zilizopo katika uzalishaji kwenye mifugo, uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili waweze kupata faida kwenye kazi zao.