Na Penina Malundo,Timesmajira
Tanzania na Urusi zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika sekta ya utalii, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuongeza fursa za utalii, biashara na uwekezaji.
Makubaliano hayo yanaenda sambamba na kuanza kwa safari za moja kwa moja za kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) zinazounganisha Moscow na Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, hatua itakayorahisisha usafiri wa watalii na wafanyabiashara kati ya masoko hayo mawili.
Katika safari hiyo ya kihistoria ya kwanza, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, ameongoza ujumbe wa Tanzania uliojumuisha Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na wadau zaidi ya kampuni 47 za utalii.
Ujumbe huo ulikutana na wadau wa sekta ya utalii kutoka Urusi kupitia mikutano ya biashara baina ya wafanyabiashara (B2B), iliyowapa fursa ya kujadiliana, kujenga ushirikiano mpya wa kibiashara na kutangaza vivutio vya kipekee vya utalii vya Tanzania kwa soko la Urusi.

Hatua hii inatarajiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka Urusi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya utalii, na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Tanzania ya kukuza sekta ya utalii na uchumi wa nchi kupitia masoko mapya ya kimkakati.



More Stories
Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi
Kiswahili Paris: Fursa Mpya, Dunia Yaungana Leo
Watatu mbaroni tuhuma mauaji ya bibi yao