June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wajenga nyumba ya watumishi kwa mapato ya ndani

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Korogwe

HALMASHAURI ya Mji Korogwe mkoani Tanga imetumia mapato yake ya ndani kujenga nyumba ya watumishi. Lengo ni kuona watumishi hasa sekta ya afya wanakuwa karibu na eneo la kutoa huduma ili kuwatumikia wananchi.

Hayo yalisemwa Juni 24, 2026 na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe (TMO), Dkt. Miriam Cheche kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda alipofika Zahanati ya Lwengera Darajani kuweka Jiwe la Uzinduzi wa nyumba hiyo ya watumishi.

“Nyumba ya watumishi (two in one) Zahanati ya Lwengera Darajani.”

Dkt. Cheche amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri ilipanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi yenye uwezo wa kuishi familia mbili (Two in one) katika Zahanati ya Lwengera Darajani iliyopo Kata ya Old Korogwe kwa gharama ya sh. 92,780,000 kupitia mapato ya ndani.

Mradi huo ulianza kwa nguvu za wananchi na kisha kuendelezwa na halmashauri, ambapo mwaka 2025 mradi ulipitiwa na mbio za Mwenge wa Uhuru, na kuwekewa jiwe la msingi.

“Lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya, na hatimaye kuboresha huduma za afya kwa ujumla. Mradi huu umetekekezwa kwa njia ya “Force Account”. Aidha, jumla ya sh. 92,780,000 zimepokelewa, ambapo sh. milioni 82 ni fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, sh. milioni sita ni fedha za Mfuko wa Jimbo, sh. 3,716,000 ni kutoka kwa wadau, na sh. 1,064,000 ni nguvu za wananchi, na mradi umekamilika kwa asilimia 100″ amesema Dkt. Cheche.

“Zahanati ya Lwengera Darajani.”

Dkt. Cheche amesema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa mustakabali wa Taifa letu. Pia, amewashukuru wananchi wa Mtaa wa Lwengera Darajani kwa kujitokeza kuchangia utekelezaji wa mradi huo kupitia nguvu kazi na michango ya fedha.

Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Mji Korogwe kupitia fedha za mapato ya ndani, imeweza kukikopesha fedha Kikundi cha Vijana cha Maguta Mkuyuni Safari (KIMAMSA) kilichopo Soko la Manundu, Korogwe mjini sh. milioni 29.4 kupitia mikopo ya asilimia 10. Kupitia mikopo hiyo, wanawake wanapata asilimia nne, vijana asilimia nne, na watu wenye ulemavu asilimia mbili.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda akiweka Jiwe la Uzinduzi Zahanati ya Lwengera Darajani.”

Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mwang’onda, mara baada ya kufika kwenye kikundi hicho Stendi Kuu ya Mabasi Korogwe, Mwenyekiti wa KIMAMSA, Gasper Chimbasana amesema kupitia mkopo huo, wameweza kununua maguta matano, huku mkopo huo ukiwa wa miaka miwili kuanzia Novemba 7, 2025 hadi Oktoba 7, 2027, ambapo rejesho kwa mwezi ni sh. 1,225,000. Hadi sasa wamerejesha sh. 14,787,500.

Chimbasana amesema lengo la kikundi ni kuboresha shughuli za usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Halmashauri ya Mji Korogwe, na kuboresha uchumi wa wanakikundi na jamii kwa kujiajiri wenyewe na kuajiri vijana wenzao.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda akitoa somo kwa vijana wa Maguta. Kulia ni Mkurugenzi Korogwe TC, Zahara Msangi.”

Mwang’onda akizungumza kwenye mkesha wa Mwenge wa Uhuru kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Boma, alisema wamejiridhisha kwa miradi yote waliyoitembelea kwa kuweka jiwe la msingi, kuizindua na kuikagus kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe, kwani yote ilikuwa na viwango vyenye ubora, na haina maelekezo yeyote.

“Vijana wakiwa kwenye Maguta kabla ya kutembelewa na Kiongozi wa Mwenge, Mwang’onda.”
“Mwang’onda alipoguswa na wimbo wa kumkumbuka Baba wa Taifa Julius Nyerere na Abeid Karume ulioimbwa na Halaiki ya Korogwe TC.”
“Mkurugenzi Korogwe TC, Zahara Msangi akipanda mti, Shule ya Msingi Matondoro.”