October 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barabara za lami Mtumba kufungua njia huduma Serikalini



Na Joyce Kasiki, Dodoma


UJENZI wa kilomita 59 za barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, unatajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya kurahisisha shughuli za kiutawala na safari za wananchi wanaofika kupata huduma katika wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema uwekezaji huo wa miundombinu unaenda sambamba na mpango wa kuweka ofisi za Serikali katika eneo moja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa umma.


Msigwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na wahariri waliotembelea Mji wa Serikali Mtumba, ambapo ameeleza kuwa mkusanyiko wa wizara na taasisi katika eneo hilo unatarajiwa kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaohitaji huduma kutoka ofisi tofauti.


Amesema Serikali pia imejenga majengo ya kisasa na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za kiutendaji, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Kwa mujibu wa Msigwa, matumizi ya mifumo ya serikali mtandao ni sehemu ya jitihada za kupunguza ulazima wa wananchi kufika ofisini kwa kila huduma, kwani baadhi ya mahitaji yanaweza kushughulikiwa kwa njia ya mtandao.


Ameeleza kuwa miundombinu ya barabara iliyojengwa Mtumba inalenga kurahisisha usafiri na kuwezesha wananchi kufika katika ofisi wanazohitaji bila usumbufu, huku mazingira ya mji huo yakitoa nafasi kwa taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake.


Aidha, amesema majengo na mpangilio wa miundombinu katika eneo hilo vinaongeza upekee wa Mji wa Serikali Mtumba, ambao unaweza kuwa sehemu ya kuvutia wageni wanaofika Dodoma.


Msigwa ametoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa kuhusu maendeleo ya mji huo kupitia vyombo vya habari, akiwashukuru waandishi na wahariri kwa kutembelea eneo hilo na kujionea uwekezaji uliofanyika.