Na Penina Malundo,Timesmajira
MFUKO wa Taifa wa huduma ndogo za kifedha (Self Microfinance Fund SELF MF) umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 138 katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, na kuwafikia wanufaika 131,312, hatua iliyochochea shughuli za kiuchumi na kutengeneza ajira 262,624 nchini.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mfuko huo jana Jijini Dar es salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Self Microfinance Fund Santieli Yona wakati wa Mkutano ulioratibiwa na Msajili wa Hazina,alisema mafanikio hayo yanaonesha mchango wa taasisi hiyo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma za kifedha na mikopo inayolenga makundi mbalimbali ya jamii.
Alisema katika kipindi hicho, mfuko umeweza kupata faida ya Sh bilioni 3.19, jambo linaloonesha uwezo wake wa kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na kutumia vizuri mtaji uliowekezwa na Serikali, huku ukiendelea kutoa huduma kwa wananchi wanaohitaji mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara zao.

Akitaja mafanikio mengine ni pamoja na utoaji wa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitatu, hatua inayochangia mapato ya Serikali na kuonesha kuwa taasisi hiyo ina uwezo wa kujiendesha kibiashara huku ikitekeleza jukumu lake la kijamii la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Aidha amesema,mfuko umeendelea kutoa mikopo ya aina mbalimbali kwa wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine ya wananchi, pamoja na kuwezesha taasisi za kifedha kama SACCOS na AMCOS kupata fedha za kukopesha wanachama wao, ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kupitia mikopo hiyo, baadhi ya wanufaika wameweza kupanua shughuli zao za biashara na kuongeza uwezo wa kiuchumi, akieleza kuwa kuna wateja walioanza na mikopo midogo na baadaye kufikia uwezo wa kukopa kiasi kikubwa zaidi.

Amesema mfuko huo pia unatoa mikopo ya maendeleo ya makazi inayowawezesha wananchi kukamilisha nyumba zao, pamoja na mikopo kwa watumishi wa umma, huku ukiendelea kubuni bidhaa zinazolenga kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali na kuongeza fursa za kujikwamua kiuchumi.
Akizungumzia miaka mitano.amesema katika mpango wa miaka mitano ijayo, mfuko unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma kwa njia za kidijitali ili wananchi waweze kupata taarifa na huduma za mikopo kwa urahisi zaidi bila kulazimika kufika katika matawi yake, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za umbali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Amesema Self pia imejikita katika kukuza matumizi ya nishati safi kwa kutoa mikopo inayowawezesha wananchi kupata majiko yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo, pamoja na bidhaa nyingine zinazolenga kulinda mazingira. Amesema hatua hiyo inaendana na juhudi za taifa za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.


More Stories
TANESCO yafunga transfoma ya mva 150 kuimarisha umeme
Barabara za lami Mtumba kufungua njia huduma Serikalini
Kawaida atoa ufafanuzi majukumu ya Chipukizi,Vijana CCM